Mliokuwa mkilalamika kukosa vitambulisho NIDA kachukueni

Nipashe
Published at 09:16 PM Jul 17 2024
Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Picha: Mtandao
Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

WAKATI Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ilipokuwa ikatangaza watu kujiandikisha kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo, wengi walikuwa wakisuasua na kuona ni suala lisilo na umuhimu.

Pamoja na wananchi kupewa elimu ya umuhimu wa kuwa na vitambulisho hivyo, mwamko haukuwa mkubwa sana.

Vitambulisho vya NIDA vina kazi kubwa na ni muhimu kuwa navyo kutokana na kuhitajika kila mwananchi anapohitaji huduma.

Kwa mfano mtu anapokwenda benki kufungua akaunti ataulizwa kitambulisho hicho, anapotaka kupata hati ya kiwanja, anapotaka huduma ya maji au umeme, atatakiwa kutoa kitambulisho cha NIDA. Na wengi wanakwama kupata huduma hizo kwa kukosa kitambulisho hicho.

Baada ya wananchi kupata adha hizo na kuamua kwenda kujiandikisha kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo, Mamlaka ya Vitambulisho ilitoa namba za utambulisho ambazo zilisaidia watu kupata huduma hizo muhimu.

Sababu za kutoa namba kwanza ni kutokana na Mamlaka kusubiri vitambulisho vichapishwe ili watu wapate kadi. 

Sasa kadi ziko tayari, lakini wananchi waliokuwa wanalalamika kucheleweshwa kupatikana kwa kadi hizo, hawajaenda kuzichukua.

Kutokana na hali  hiyo Mamlaka hiyo imetoa angalizo kwamba itafika hatua watasimamisha utaratibu wa watu kupatiwa huduma kwa kutumia namba za utambulisho (NIN), endapo wananchi wataendelea kupuuza kwenda kuchukua vitambulisho vyao ambavyo tayari vimeshatoka.

Mamlaka hiyo imebaini kuwapo mrundikano mkubwa wa vitambulisho hivyo katika ofisi za serikali za mitaa, kata, vitongoji, vijiji, wilaya na mikoa, kutokana na wahusika kutokwenda kuvichukua, huku Mkoa wa Dar es Salaam ukitajwa kuongoza kutokana na wengi kutegemea kutumia namba walizopatiwa awali.

Oktoba 2023, Mamlaka ilianza uzalishaji mkubwa wa Vitambulisho vya Taifa na kuvisambaza kwa wingi katika maeneo mbalimbali katika mikoa, wilaya na vijiji.

Hiyo ilikuwa ni kukidhi mahitaji ya wananchi ambao walikuwa wakilalamika kuwa hawana vitambulisho na wanakosa huduma.

Baada ya kusikia malalamiko ya wananchi, Mamlaka ilipata imani kwamba endapo watazalisha na kusambaza, ndani ya muda mfupi watajitokeza kwa wingi na kuchukua, akieleza kuwa kwa sasa hali ni tofauti na walivyotarajia kwakuwa kasi ya wananchi sio kubwa hasa katika maeneo ya mijini.

Mkoa wa Dar es Salaam umebainika kuwa uko chini kwa takwimu za kuchukua vitambulisho kuliko mingine, licha ya kuongoza kwa malalamiko ya watu kuonyesha uhitaji.

Alisema tatizo hilo linachangiwa na watu kuendelea kupatiwa huduma kwa kutumia namba za utambulisho wa taifa na kwamba hiyo inasababisha wananchi kutokuona haja ya kwenda kuchukua kitambulisho hata kama anajua kuwa kimetoka.

Tatizo lingine ni watu kuhama katika maeneo waliyojiandikishia ikiwamo watumishi wa umma na wanafunzi wa elimu ya juu ambao wameshamaliza masomo wameajiriwa katika maeneo mengine, huku nyuma vitambulisho vimetoka inakuwa shida kuja kuchukua. 

Utaratibu wa kuchukuliwa kitambulisho inahitaji kuzingatia mhusika kutakiwa kuandika barua ya kumtambulisha atakayekwenda kumchukulia na ataweka sahihi yake, anaeenda kuchukua naye ataandika nyingine kwamba ataenda kumchukulia ndugu yake, ataandika majina yake, namba ya simu na kivuli cha namba ya utaifa.

Wananchi waache kisingizio cha kutokuchukua kitambulisho kutokana na umbali kwa kuwa mamlaka imeweka utaratibu mzuri wa kuchukuliana.

Lengo la serikali la kuweka utaratibu wa kila mwananchi kuwa na kitambulisho cha utaifa ni pamoja na kuimarisha usalama na kuwa na taarifa muhimu za kila Mtanzania.