KATIKA juhudi za kuwafikia na kuwahudumia wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha masuala ya usawa wa kijinsia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kinajenga kituo maalumu kwa ajili ya wanafunzi, wafanyakazi na wageni.
Kituo hicho kitashughulikia masuala mbalimbali yanayohusiana na jinsia na ulemavu, kutoa msaada wa kisaikolojia, vifaa saidizi na elimu kuhusu haki za binadamu na ukatili wa kijinsia ni mradi unaongeza pia miundombinu rafiki kwa wenye mahitaji maalumu.
Kujenga kituo hicho kitakachotoa huduma kwa wakati mmoja yaani ‘one-stop center’ ni juhudi za UDSM kuimarisha elimu jumuishi, kuweka mazingira salama yanayowashirikisha wote na kutoa kipaumbele zaidi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Kituo hicho, kinajengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia (WB) ambayo inazisaidia taasisi 23 za elimu ya juu, kujenga miundombinu ya elimu na huduma muhimu kwa ajili ya wanafunzi kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Jinsia UDSM, Dk. Lulu Mahai, anaiambia Nipashe kuwa dhamira ya kituo hicho ni kuhudumia kwa ukarimu, ukaribu na ufanisi wanafunzi na wadau wenye ulemavu wa aina mbalimbali kwa kuwapatia huduma kulingana na mahitaji yao maalum, ikiwamo usaidizi wa kijamii na kitaaluma.
“Kituo hiki kitatoa nafasi kwa wanafunzi wote wenye ulemavu, aidha na wenye kuhitaji msaada wa kisaikolojia, na huduma nyingine kwa wanafunzi wa kawaida ili kukabiliana na ukatili wa kijinsia, tutahakikisha wanapata msaada unaostahili ili kuimarisha elimu na kufanikisha malengo yao ya kitaaluma, kituo hiki ni sehemu muhimu ya mpango wa chuo kuhakikisha ushirikishwaji wa makundi yote katika elimu ya juu,” anasema Dk. Lulu.
Anaongeza kuwa kituo hicho kitakuwa na dawati maalum la kushughulikia changamoto zinazohusiana na jinsia, ili kuhakikisha mazingira yasiyo na unyanyasaji wa kijinsia na kuweka mbele haki na usawa wa kijinsia, anasema chuo kimejitolea kuhakikisha kuwa mahali salama dhidi ya unyanyasaji wa aina yoyote.
Anasema chuo kilianza kupokea watu wenye ulemavu mwaka 1978 wakiwa wanaume, anasema waliendelea kupokea na hadi sasa wanao zaidi ya 20.
HISIA ZA WALENGWA
Mwakilishi wa WB, Profesa Roberta Malee, anaipongeza UDSM kwa kujenga kituo cha kwanza cha aina hiyo nchini, akisema ni jambo la kimapinduzi siyo kwa Tanzania, bali Afrika pia.
“Tunafurahi kuona mnafanya mapinduzi makubwa kwenye elimu jumuishi tuna matumaini mradi huu utaboresha maisha ya wanafunzi wote kwa kutoa nafasi za kipekee za kujifunza na kukua katika mazingira yanayowajali.” Anasema Prof. Roberta.
Erick Nyanda, mwanafunzi mwenye ulemavu chuoni hapo, anaelezea matumaini makubwa kuhusu mradi huo akisema kituo hicho kitakuwa kiunganishi cha wanafunzi wenye ulemavu na wale wasio nao.
Anasema kitawawezesha wote kubadilishana mawazo, kushiriki michezo na mazoezi mbalimbali ya viungo, jambo litakalokuza umoja na ushirikiano miongoni mwao.
“Tutaweza kupata msaada wa moja kwa moja kwa mahitaji yetu maalum, ikiwamo ushauri wa kisaikolojia na vifaa vya kisasa vya teknolojia vya kujifunza,” anasema Erick.
Mashukura Kabwogi, mtafsiri wa lugha za alama UDSM, anasema kituo hicho kitawasaidia wanafunzi wenye ulemavu kupata huduma stahiki na kujifunza bila vizuizi.
Mradi wa ujenzi wa kituo hiki ni sehemu ya Mpango wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), mpango wa miaka mitano unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kuimarisha elimu ya juu.
Dk. Liberato Haule, Naibu Mratibu wa HEET UDSM, anasema utagharimu Dola za Marekani milioni 47.5 (sawa na shilingi bilioni 109) kuboresha miundombinu ya elimu, ujenzi wa madarasa, mabweni, maabara, na vituo vingine katika kampasi mpya za chuo hicho zilizopo mikoa ya Kagera, Lindi na Mtwara.
Aidha, anasema katika kuboresha utoaji wa elimu, wametengeneza mitaala 98 ambayo ipo kwenye hatua za mwisho za kupata ithibati kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania(TCU) ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Anaongeza kuwa tayari walimu 38 wamepata mafunzo ya kujifunza teknolojia mbalimbali viwandani na pia wataalamu 31 kutoka sekta mbalimbali wameshiriki kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa UDSM.
Anasema kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimefanya juhudi mbalimbali kutekeleza sera, sheria, na miongozo inayohusiana na haki za watu wenye ulemavu, hususan katika elimu ya juu.
UDSM imetekeleza, Sera ya Taifa ya Watu Wenye Ulemavu (2004), ambayo inasisitiza umuhimu wa kuwezesha wenye ulemavu kujumuishwa katika jamii, anaongza Dk. Haule.
Chuo kimeandaa mikakati inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia, ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko katika mitaala na kutoa vifaa vya kusaidia wanafunzi wenye ulemavu, anasema.
Naibu Mratibu wa HEET UDSM, anasema chuo kimezingatia pia Sheria ya Watu Wenye Ulemavu (2010), ambayo inalinda haki zao katika mazingira ya elimu.
Kadhalika, anasema kimetimiza matakwa ya Katiba ya Tanzania (1977) inayotaka kuwapo misingi ya haki za binadamu, ikiwamo haki za watu wenye ulemavu, na inasisitiza umuhimu wa usawa katika kupata elimu na huduma nyingine.
Akizungumzia mradi wa HEET na mustakabali wa elimu Tanzania, anasema unatarajiwa kuwa na matokeo makubwa kwenye elimu ya juu kwa kuboresha miundombinu, vifaa na mitalaa ya kisasa ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu inayolingana na mahitaji ya kiuchumi ya sasa na ya baadaye.
Aidha, Dk. Haule anasema mradi huo pia unalenga kuajiri walimu, watafiti, na wasimamizi wenye ujuzi na kufundisha kwa viwango vya kimataifa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED