KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Amos Makalla ametoa wito kwa wagombea kwamba CCM inahitaji subira na watakaokatwa licha ya kushinda kura za maoni wasiseme neno la kukatwa, badala yake wawe na uvumilivu kwakuwa muda wao utafika.
Makalla ameyazungumza hayo leo mkoani Dar es Salaam katika mkutano wa chama Wilaya ya Kinondoni, huku akiwatakia kila la kheri wale wote waliohamia vyama vingine, akidai kuwa ni suala la muda tuu watarudi.
Pia amewapongeza baadhi ya wagombea ambao majina yao yalikatwa na bado wanaendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za chama hicho, akijitolea mfano yeye mwenyewe kwamba kuna kipindi aligombea na kushinda kwa kishindo lakini jina lake halikurudi.
“Tunawatakia kila la kheri waliokosa uvumilivu, wako ambao hata uteuzi haujafanyika wakahamia mtaa wa pili siku ya tatu wakageuza tena CCM, niwape salamu hao waliowaokoteza tumewaazima tuu wagombea watarudi Chama cha Mapinduzi,” alisema na kuongeza:
“Kuna wengine hata vikao hatujakaa niliona wanakaribishwa siku mbili jamaa akarudisha kadi akarudi CCM, hivyo niwaombe kuweni watulivu tuna uchaguzi mwakani,” amesema Makalla.
Aidha, amesema uchaguzi wa awamu hii hauna kupita bila kupingwa, hivyo waombea na wanachama wa chama hicho wasibweteke, akisisitiza kwamba wako imara na hawatalala.
Amesisitiza kwamba watahakikisha hata pale watakapokuwa wako pekeyao watafanya kampeni na kuhakikisha wagombea wao wanapata kura za ndio.
“Anaesubiri kumuangusha mgombea wa CCM kwa kura za hapana ni sawa na mtu anaesubiri ndege bandarini badala ya ‘Airport’ wanaccm nchini kote tuchangamke hakuna neno ‘Mama’ tukamilishe hiyo kazi, mahali patakapothibitika tuko sisi tutafanya kampeni ya kutosha wagombea wetu wote wapite kwa kishindo,” amesema Makalla.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED