MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango ameelekeza Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini (TACAIDS) kwa kushirikiana na wizara za kisekta, wadau na jamii kwa ujumla kuweka mkazo katika kudhibiti mazingira yanayochochea maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU).
Alielekeza hayo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika Kitaifa kwenye Uwanja wa Majimaji, mjini Songea, mkoani Ruvuma.
Alitaja vigingi vilivyopo katika kutokomeza UKIMWI nchini vinajumuisha jamii kuwa na mtazamo hasi dhidi ya walioambukizwa virusi hivyo, hata kuchangia kurudisha nyuma jitihada za kupambana na UKIMWI.
Alisema mtazamo hasi huwafanya wahitaji kushindwa kupata huduma kwa kuonekana kuwa hawastahili na hivyo kutengwa. Alionya kuwa unyanyapaa husababisha woga unaoathiri upimaji kwa hiari na upatikanaji huduma nyingine kama za unasihi pamoja na ARV kwa wale wanaoishi na VVU.
Aliwataka vijana kujitambua, kujithamini na kutunza maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kwa kuwa kasi ya maambukizi katika kundi hilo inaonekana kuwa kubwa. Takwimu za hali ya UKIMWI nchini zinaonesha kundi la vijana na hasa wa kike liko katika hatari zaidi ya kupata maambukizi mapya ya VVU.
Makamu wa Rais aliwataka wananchi kuzingatia maudhui ya elimu inayotolewa kupitia kampeni mbalimbali kwa ajili ya kubadili tabia, kuachana na mila zinazoweza kuwa vichocheo vya maambukizi na kuendelea kujikinga na maambukizi mapya ya VVU.
Alisema hali ya maambukizi mapya inaonekana kuchochewa zaidi na mazingira na tabia hatarishi hususan ulevi uliopindukia, ngono zembe, kuwa na wapenzi wengi na matumizi ya dawa za kulevya.
Alisema mapambano dhidi ya UKIMWI yaliyoanza takriban miongo minne iliyopita, yamepata mafanikio. Matokeo ya utafiti wa viashiria vya VVU na UKIMWI uliofanyika mwaka 2022/23, yanaonesha maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye umri kuanzia miaka 15 ni watu 60,000 kwa mwaka. Kiwango cha ushamiri wa VVU kitaifa ni asilimia 4.4 ambapo jumla ya watu 1,548,000 wanaishi na VVU.
"Kiwango cha ushamiri wa VVU kwa wenye umri kuanzia miaka 15 na zaidi kwa upande wa Tanzania Bara ni asilimia 4.5 na asilimia 0.4 kwa upande wa Zanzibar. Viwango vya ushamiri kwa mikoa ya Tanzania Bara vinaanzia asilimia 1.7 (Kigoma) hadi asilimia 12.7 (Njombe). Mikoa mitatu ya Mbeya, Iringa na Njombe ina viwango vya ushamiri zaidi ya asilimia tisa (9) ambayo ni mara mbili ya kiwango cha kitaifa," alisema.
Awali Waziri wa Afya, Jenista Mhagama alisema wizara itaendelea kufanya maboresho ya kuhakikisha uamuzi wa kuunganisha mwitikio kwa kujumlisha uratibu wa magonjwa ya ngono, homa ya ini na UKIMWI kama vihatarishi vinavyofanana na vinavyofananishwa katika njia za maambukizi, kwa pamoja vinawekewa mkakati madhubuti wa kupambana navyo ili kuimarisha afya za watanzania.
ZANZIBAR
Akiwa mkoa wa Kusini Pemba jana, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, alisema changamoto zinazohusiana na haki za binadamu katika upatikanaji huduma za UKIMWI zinachangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha juhudi za serikali na ulimwengu kwa ujumla katika kumaliza tatizo la UKIMWI.
Alisema changamoto hizo, ukiwamo unyanyapaa na watu kulazimishwa kupima, na unyanyasaji wa kijinsia hupelekea watu kukosa na kuogopa kuzifikia huduma za kujikinga na VVU pamoja na za matibabu kwa wanaoishi na VVU.
Makamu wa Rais alisema hofu ya unyanyapaa inasababisha watu waogope kwenda vituo vya afya kuchunguza afya zao na ni miongoni mwa yanayosababisha wanaoishi na VVU kushindwa kutumia dawa ipasavyo.
Othman pia alikosoa tabia ya baadhi ya mashirika na taasisi kuwalazimisha wafanyakazi wao hasa inapotokea haja ya kuongezwa mikataba, kupimwa kwa lazima, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za afya Zanzibar.
"Mbaya zaidi ni katika baadhi ya vituo vya afya hapa Zanzibar kuwalamisha wananchi kupima VVU kabla ya kupatiwa huduma muhimu za afya wanazozihitaji, ukiwamo upasuaji licha kwamba kisheria uchunguzi huo unatakiwa kuwa wa hiari," alisema.
Alionya kuwa hali hiyo inaweza kuchochea maambukizo mapya katika jamii kwa kuwa watu wenye wasiwasi wa kuishi na VVU hulazimika kuzikimbia huduma ambazo ni muhimu katika kuimarisha afya zao na kusaidia kupunguza maambukizo kwa watu wanaowazunguka na jamii kwa jumla.
Hata hivyo, Makamu wa Rais alisema Zanzibar haina budi kujipongeza kwa mafanikio ya kudibiti kiwango cha maambukizo ya VVU kubaki chini ya asilimia moja na kwamba utafiti wa karibuni unaonesha kwamba ni asilimia 0.4 ya wakazi wa Zanzibar wanaoishi na VVU.
Alisema hatua hiyo pia imesaidia kupunguza vifo vinavyotokana na maradhi ya UKIMWI Zanzibar kutoka 519 mwaka 2020 hadi watu 362 mwaka 2023 na kupunguza idadi ya maambukizo mapya kutoka watu 274 mwaka 2020 hadi maambukizo 190 kwa mwaka 2023.
Othman alisema kuwa ifikapo mwaka 2025, Zanzibar inatarajia kuungana na ulimwengu kufikia shabaha ya 95 tatu, hata kumaliza kabisa tatizo la UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Alisema matumaini hayo yanatokana na kwamba hadi kufikia mwaka 2024, shabaha ya 95 ya kwanza ya kujitambua tayari imefikiwa kwani aslimia 90 ya wanaokisiwa kuishi na VVU wanajitambua na 95 ya pili ni kwamba hadi kufikia Septemba 2024 asilimia 98 ya wanaojitambua wanaendelea kutumia dawa na ile 95 ya tatu ni kwamba asilimia 95 ya wanaotumia dawa, wameweza kupunguza makali ya virusi.
Makamu wa Rais alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano ya serikali na wadau wa maendeleo, akiwashukuru wadau hao kutokana na ushirikiano wao pamoja na misaada ya kiufundi na fedha wanazotoa katika kupambana na tatizo la UKIMWI nchini.
Hata hivyo, alielekeza kuongeza nguvu katika kukabili ipasavyo mazingira hatarishi yanayoweza kuchangia maambukizo mapya na kwamba ni wajibu wa kila mmoja kuishi kwa tahadhari ya kujilinda dhidi ya VVU. Alihimiza jamii kushikamana na kuwa na utaratibu bora wa maelezi ili watoto na vijana wasitumbukie katika vishawishi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Harous Said Suleiman alisema shughuli mbalimbali za kutoa elimu na kuhamasisha watu kupima kujua hali yao zilifanyika kwa ufanisi mkubwa kuelekea maadhimisho hayo.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mapambano dhidi ya UKIMWI (UNAIDS), Dk. Gorge Loy alisema bado zipo changamoto kwa watu walio na VVU kufikiwa na huduma, huku unyanyapaa dhidi yao ukiendelea katika jamii.
Mwenyekiti wa Tume ya Ukimwi Zanzibar, Dk . Ali Salim alisema kuwa katika kufikia malengo ya mapambano hayo, kuna haja kuangaliwa na kubadilishwa sheria zinazosimamia maradhi ya UKIMWI kutokana na suala la unyanyapaa na ubaguzi kuendelea ndani ya jamii dhidi ya watu wanaoishi na VVU.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED