Risiti feki za EFD zashtua miradi ya taasisi za serikali

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 10:25 AM Dec 02 2024
Risiti za EFD.
Picha:Mtandao
Risiti za EFD.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Morogoro imesema lipo wimbi la risiti za kielektroniki zisizo halisi (feki) zinazotolewa kwenye miradi inayotekelezwa na taasisi za serikali huku baadhi ya wanaofanya mchezo huo wakiwa wazabuni na makandarasi mkoani humo.

Imesema risiti hizo zisizo sahihi mara nyingi pia zimekuwa zinatolewa yanapofanyika malipo ya ununuzi kutoka kwa  watoa huduma mbalimbali na kusababisha serikali kushindwa kupata kodi yake.

Meneja Msaidizi wa TRA Mkoa wa Morogoro, Chacha Gotora alisema mwishoni mwa wiki mjini hapa kuwa baada ya kupata malalamiko hayo kutoka taasisi za serikali, wameamua kutoa mafunzo ya kuhakiki risiti sahihi kabla hawajafanya malipo yoyote kwa watoa huduma.

"Kuna baadhi ya kesi ambazo tulikuwa tukizipata kutoka kwa wenzetu wa taasisi za umma kuja kuhakiki risiti na zikaonekana kuna wimbi la kupelekewa risiti zisizo sahihi, hivyo kama TRA tumeamua kutoa elimu kwa viongozi wa taasisi hizo ili wajue risiti sahihi inatakiwa iweje na vitu vya kuitambua," alisema Chacha.

Alisema mafunzo hayo yatasaidia taasisi hizo za serikali zinazotekeleza miradi mbalimbali kuwabaini wazabuni na watoa huduma wengine wanaotoa risiti feki na kuwachukulia hatua wale watakaobainika kuziandaa.

Julieth Hamza, Mhasibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), alisema changamoto wanayopata ni uelewa wa wazabuni kuhusu Kodi ya Zuwio pale wanapofanya ununuzi na kukatwa kodi hiyo.

"Kukosekana kwa elimu ya Kodi ya Zuwio kumekuwa kunatusababishia matatizo kwa kuwa mzabuni ukimwambia nimekukata hiyo kodi, hataki kukupa risiti ya jumla ya fedha zote badala yake anatoa risiti ya fedha uliyompa," alisema Julieth.

Ofisa Ununuzi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Abdulkarim Mushi, alisema changamoto inayosababisha malipo ya wazabuni kuchelewa ni pamoja na utekelezaji kulingana na bajeti iliyotengwa pamoja na kutaka mahitaji ambayo hayajatengewa bajeti husika na kuchelewesha malipo.