Mchakato kupandisha viwango vya ufaulu waanza

By Getrude Mpezya , Nipashe
Published at 10:34 AM Dec 02 2024
Mkurugenzi Uthibiti Ubora wa Shule wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ephrahim Simbeye.

SERIKALI imeanza kuwanoa wadhibiti ubora wa elimu ambao watafanya kazi ya kupandisha viwango vya ufaulu na kuzalisha wanafunzi wa masomo ya amali.

Mkurugenzi Uthibiti Ubora wa Shule wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ephrahim Simbeye, akizungumza mwishoni mwa wiki Jijini Arusha, alisema walengwa wa mafunzo hayo wanatarajia kuchochea mabadiliko katika sekta ya elimu nchini.

"Tumewaleta kujinoa kuhusu elimu ya amali ili kuwawezesha kuboresha kiwango cha elimu ya vitendo na kuzalisha wanafunzi watakaoweza kujitegemea kimaisha baada ya kumaliza masomo. 

"Niwasihi wathibiti ubora kuwasikiliza kwa umakini watoa mada ili elimu hiyo iwasaidie na wengine waliobaki ofisini kwa lengo la kuboresha kiwango cha elimu na kuingia katika mashindano ya kikanda na kidunia.

...Ndugu zangu nyinyi ndiyo watu wa viwango wa elimu yetu na jiicho la Wizara. Mkishirikiana na kukaa pamoja naamini mabadiliko yatakuwa makubwa; tunategemea mafunzo haya yawe endelevu na yenye kuleta tija, msiwe wachoyo wa kuwaelimisha wengine ili kufikia malengo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kama inavyotakiwa." alisema 

Hatahivyo, aliwataka kuthibiti ubora wa ndani ya shule, kushirikisha jamii katika masuala ya maendeleo ya elimu, kusimamia unasihi na ushauri nasaha kama ilivyo katika suala la maadili.

"Nawakumbusha kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo hapa Mkoa wa Arusha ili kuliingizia taifa mapato, hii inawezekana kukifanyika utaratibu mzuri ili mkafurahie mandhari na utajiri uliopo katika vivutio hivyo" alisema Simbeye.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Ualimu, Huruma Mageni alisema mafunzo hayo ni muhimu kutokana na umuhimu wa elimu ya amali inayolenga kuleta chachu na matokeo makubwa katika teknonojia na kujitegemea.

"Pongezi zetu ziwaendee wawezeshaji na maofisa kamisheni kutoka Wizara ya Elimu, NACTEVATE na VETA watakao fundisha mpangilio na mtaala wa amali na fani za amali, utaratibu wa kusajiri shule za amali, muundo wa kuandika tathmini ya amali na mengine mengi" amefafanua Mageni.

Mthibiti Ubora Elimu wa Halmashauri ya Wilaya Newala mkoani Mtwara, Rashid alisema wawezeshaji wameanza kutoa mwanga na maelekezo kuhakikisha elimu ya amali inaboreshwa.

"Kwa upande wangu changamoto ninazoziona ni upungufu wa walimu katika shule za amali, vifaa vya kufundishia na miundombinu michache kwa maana ya maktaba na maabara" alisema Rashid. 

Mthibiti Ubora kutoka Halmashauri ya Handeni Mkoani Tanga, Telesia Kapinga alisema mafunzo hayo yatawapatia elimu ya kujitegemea na kuanzisha viwanda vidogovidogo.

Mafunzo hayo yatafungwa Desemba 02 na yamebeba kaulimbiu isemayo "Utoaji wa elimu bora ya amali hutegemea tathmini makini ya ufundishaji na ujifunzaji".