Ouma afunguka sababu za kukubali kujiunga Singida BS

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:37 PM Dec 02 2024
KOCHA mpya Msaidizi wa Singida Black Stars, David Ouma.
Picha:Mtandao
KOCHA mpya Msaidizi wa Singida Black Stars, David Ouma.

KOCHA mpya Msaidizi wa Singida Black Stars, David Ouma, amezungumza kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo, akisema malengo makubwa na ushindani wanaouonesha wachezaji wa timu hiyo kwenye Ligi Kuu, ndiyo uliomfanya kukubali kutua kwenye kikosi hicho.

Akizungumza juzi baada ya kujiunga rasmi na kikosi hicho, Ouma, alisema alikuwa na ofa nyingi mkononi za klabu mbalimbali hapa nchini, lakini ameichagua timu hiyo kutokana na kuwa na malengo makubwa na ya ushindani, huku mwenyewe akiwa ni mshindani kamili.

"Malengo waliyokuwa nayo yamenipa matamanio makubwa ya kujiunga nao, kulikuwa na timu nyingi zilikuwa zikinihitaji, lakini nimeichagua Singida Big Stars, wana malengo makubwa, mimi napenda kushindana.

"Na walipokuja walikuja moja kwa moja na kuniambia nini wanataka na mimi nikawapa ya kwangu tukaelewana. Niwashukuru wachezaji, viongozi na mashabiki wa Singida Black Stars, nimekaribishwa vizuri, kilichobaki sasa ni kufanya kazi," alisema Ouma.

Kabla ya kujiunga na timu hiyo, Ouma raia wa Kenya, alikuwa na kikosi cha Coastal Union msimu uliopita, ambapo alikiwezesha kushika nafasi ya nne mwishoni mwa Ligi Kuu msimu uliopita na kucheza michuano ya kimataifa, Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Hata hivyo, Coastal Union ilitolewa hatua za awali kwa kufungwa kwa jumla ya mabao 3-0 na Bravo do Maquis ya Msumbiji, iliyocheza na Simba Jumatano iliyopita kwenye michuano hiyo.

Ilichapwa mabao 3-0 ugenini, kabla ya kutoa suluhu nyumbani, matokeo ambayo yalimfanya kuondoshwa kwenye timu hiyo, akiwa kocha wa kwanza kutimuliwa kwa timu za Ligi Kuu.

Singida Black Stars hivi karibuni iliwasimamisha makocha wake wawili, Patrick Aussems na Danis Kitambi kutokana na kile ambacho uongozi ulisema ni mwenendo usioridhisha wa timu hiyo.

Licha ya kusema imewasimamisha, lakini tayari klabu hiyo imemtangaza Ouma kama kocha msaidizi, huku pia kukiwa na tetesi za kocha wa zamani wa Yanga, Miguel Gamondi, kushika nafasi ya ukocha mkuu.