KOCHA Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesifu kiwango cha kiungo mshambuliaji, Clatous Chama, akisema ni cha hali ya juu na ndiye aliyebadilisha mchezo kiasi cha kushinda mabao 2-0 katika mechi ya juzi dhidi ya Namungo iliyopigwa Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.
Kocha huyo pia amesema ameridhishwa na kiwango cha wachezaji wake akisema vinapanda taratibu ingawa bado havijawa kwa asilimia zote, hasa upande wa pumzi na utimamu wa mwili.
Yanga imepata ushindi huo kwa mara ya kwanza, baada ya kupoteza michezo mitatu mfululizo, miwili ya Ligi Kuu Bara, ikifungwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC, Novemba 2 na mabao 3-1, Novemba 7, mwaka huu na kisha kuangukia pua kwa kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Al Hilal ya Sudan kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Angalau leo nimeridhishwa na kiwango cha wachezaji wangu, katika mchezo wa leo nimeona wameanza kukaa sawa. Najua tumepata pointi tatu, lakini bado tunatakiwa kupandisha tena viwango vyetu juu na hasa upande wa pumzi na utimamu wa mwili, si rahisi lakini kidogo kidogo tutakaa sawa, kuna vitu vingine vya kufanya kama kocha, muhimu tumeshinda mchezo huu, ilikuwa muhimu sana kwetu kwanza kushinda kuliko kitu kingine," alisema kocha huyo ambaye ni mchezo wake wa kwanza kuiongoza Yanga kwenye Ligi Kuu, lakini wa pili kwa michezo yote.
Kocha huyo raia wa Ujerumani aliwapongeza Namungo akisema ni timu nzuri na imewapa wakati mgumu.
"Nawapongeza pia wapinzani wetu ni timu ngumu, walikuwa wanakaa nyuma wengi na wakishambulia mbele wakiwa watu wanne, ilikuwa ngumu kukabiliana nao," alisema.
Hakusita kumpa maua yake, Chama, akisema ni mchezaji maalum, kwani kuingia kwake kuliibadilisha kabisa timu na yeye ndiye aliyetoa 'asisti' iliyotengeneza mabao yote mawili kwenye mchezo huo.
Chama ameingia na kuibadilisha timu, ametoa 'asisti' mabao yote mawili, ni mchezaji mzuri sana, hivyo wachezaji wengine wanapaswa kuboresha viwango vyao, ingawa najua kikosi kina wachezaji wenye uwezo wa juu," alisema kocha huyo.
Yalikuwa ni mabao ya Kennedy Musonda na Pacome Zouzoua, yaliyoifanya Yanga kufikisha pointi 27, sawa na Azam FC, zote zikiwa na mabao 16 zikiruhusu manne, lakini 'Wanajangwani' hao bado wako nafasi ya tatu kwa alfabeti, ingawa imecheza mechi 11, huku 'Wanalambalamba' wakiwa na michezo 12, jana wakitarajia kucheza dhidi ya Dodoma Jiji.
Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda, ambayo timu yake imepoteza mchezo wa tatu mfululizo, amesema ubora wa wachezaji wa Yanga ndiyo ulioamua mechi.
"Nimekubali matokeo, si mazuri, lakini ni ya mpira, niseme tu ubora wa wachezaji wa Yanga umeamua mechi, naendelea kuiboresha timu, siku za mbele itakaa vizuri," alisema Mgunda.
Kipigo hicho kinaifanya Namungo kukaa nafasi ya 14, ikicheza mechi 12 na kujikusanyia pointi tisa tu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED