Zigo la ukatili wa kijinsia watupiwa wenyeviti S/Mitaa

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 03:19 PM Nov 30 2024
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga Rose Manumba akizungumza na Wenyeviti wa vijiji, Vitongoji na wajumbe wake wa kata za Mwalugului, jana, Isaka na Mwakata wakati wa hafla ya kuwaapisha.
PICHA; SHABAN NJIA.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga Rose Manumba akizungumza na Wenyeviti wa vijiji, Vitongoji na wajumbe wake wa kata za Mwalugului, jana, Isaka na Mwakata wakati wa hafla ya kuwaapisha.

WENYEVITI wapya wa serikali za vijiji na vitongoji katika Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga,wametwishwa zigo la kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyotokana na mila na desturi potofu zinazosababisha mabinti wengi vijijini kukatisha ndoto zao za kielimu kwa kuozeshwa kwa tamaa za wazazi za kutaka mali.

Aidha halmashauri hiyo ina jumla ya viongozi wa serikali za mitaa 2,302 kati yake wenyeviti wa vijiji 92, vitongoji 389, wajumbe mchanganyiko 1,085 pamoja wajumbe wa kundi la wanawake 736 na kila mmoja wao anatakiwa kuwa sehemu ya mapambo ya ukatili wa kijijnsia ili kuwapatia unafuaa wanawake na watoto. 

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Rose Manumba aliyabainisha haya wakati wa hafla fupi ya kuwaapisha wenyeviti hao kutoka kata za Mwakata, Jana, Mwalugulu na Isaka kiapo cha Uaminifu na kutunza siri pamoja na utiii na uadilifu, iliyofanyika katika kata ya Isaka. 

Alisema, vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa chanzo kikubwa cha kukatisha ndoto za kielemu za mabinti kwa wazazi na walezi kuendeza mila, tamaduni na desturi potofu za kuwaozesha wakiwa na umri mdogo kwa kupeana na mifugo, linatakiwa kukemewa vikali lisiendelee kujitokeza kwenye jamii. 

Manumba alisema, wenyeviti wa serikali za vijiji, vitongoji pamoja na wajumbe wake wanatakiwa kupambana na kuhakikisha hakuna vitendo vya ukatili vinavyoweza kutokea kwenye maeneo yao na kuhakikisha kutokuwa sehemu ya vitendo hivyo kwa kigezi cha kujipatia fedha kwani nafasi walizonazo sio sehemu ya chanzo cha mapato ya familia zao. 

“Wenyeviti mnaotoka maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa madini hakikisheni mnaongeza nguvu katika kuhakikisha hakuna utoroshaji wa madini ili kutokupoteza mapato. Vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa wananchi wanaozunguka migodi vikomeshwe mara moja na wahusika wanachukulia hatua na kuwafikisha vyombo vya sheria”Aliongeza Manumba. 

Hata hivyo aliwataka pia kutokuwa chanzo cha migogoro ya ardhi kwa kujihusisha na uzwaji wa viwanja kwa zaidi ya wananchi wawili kwa tamaa ya kutaka fedha, kwani Ofisi za serikali za vijiji na vitongoji sio chanzo cha mapato ya halmashauri wale familia na wale watakaobainika watachukuliwa hatua za kinidhamu. 

Ofisa Rasirimali watu na utawala wa Halmashauri Merry Nziku alisema, kila mmoja atakiwa kufanyakazi kwa kuzingatia viapo walivyoapa mbele ya hakimu nasio kuwa sehemu ya kutoa siri za wananchi hadharani na kuwa chanzo cha migogoro na wale watakaobainika wafahamu watachukulia hatua ikiwemo kuvuliwa Madaraka. 

Mwenyekiti wa kijiji cha Magunhuwa kata ya Mwakata Salumu Mohamed alikili kwenye eneo lake kuwepo kwa vitendo vya ukatili na ameshiriki mara kadhaa kuvunja ndoa za utotoni na baadhi ya wahusika wameshawafikisha kwenye vyombo vya sheria na kufungwa hivyo ajenda ya kupambana na vitendo hivyo inaendelea. 

Nae Mwenyekiti wa Isaka Bandari Samson Mwandu alisema, atahakikisha hajihusishi na uzaji wa viwanja na kesi za migogoro ya ardhi zitazokuwa zinafika kwake atawaelekeza wananchi kwenye mabaraza ya kata kutafuta haki kisheria na vijana wanaoomba kazi bandarini atashirikiana nao kuhakikisha wanapata.