Jeshi la Polisi Tanzania limesema Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya chama cha ACT- Wazalendo, Abdul Nondo alitelekezwa jana usiku katika fukwe za Coco.
Taarifa hiyo ya Polisi iliyotolewa leo Jumatatu, Desemba 2, 2024 na msemaji wake, David Misime imeeleza baada ya kutelekezwa katika fukwe hizo, aliomba msaada wa bodaboda kumfikisha katika ofisi za chama chake Magomeni, Dar es Salaam.
"Desemba mosi, 2024 majira kama saa nne na nusu usiku Abdul Omary Nondo ambaye tulikuwa tunamtafuta kwa kushirikiana na watu mbalimbali, wakiwepo viongozi wake wa chama cha ACT Wazalendo baada ya kukamatwa na kuchukuliwa kwa nguvu pale kituo cha mabasi cha Magufuli ameeleza alitelekezwa maeneo ya fukwe za Coco (Coco Beach) Kinondoni, Jijini Dar es Salaam na watu asiowafahamu.
"Baada ya kutelekezwa alisimamisha bodaboda na kumwelekeza amfikishe katika ofisi za chama chake zilizopo Magomeni, Jijini Dar es Salaam na walifika muda wa saa tano usiku,” imeeleza tarifa hiyo na kuongeza kuwa alionana na viongozi wake na kupelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.
ILIVYOKUWA JANA
Jana baada ya taarifa za kutekwa kwa Nondo kusambaa chama chake kiliwataka wanaomshikilia kumwachia haraka kwani kinajua mmiliki na lilikoegeshwa gari lililotumika kumteka.
Nondo anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana jana alfajiri kwenye Stendi ya Mabasi ya Magufuli, iliyoko Mbezi Loius, wilayani Ubungo, Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi lilisema linachunguza tukio hilo ili kubaini waliomchukua Nondo, wakitumia gari lenye rangi nyeupe aina ya Toyota Landcruizer.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Naibu Katibu wa Haki za Binadamu na Vyombo vya Uwakilishi wa Wananchi wa chama hicho, Mbarala Maharagende, Nondo alitekwa alfajiri ya jana na watu wasiojulikana, akitokea mkoani Kigoma alikokuwa sehemu ya viongozi wa kitaifa walioongoza kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mikoa ya magharibi mwa nchi.
Maharagande alidai Nondo aliwasili Stendi ya Mabasi ya Magufuli kwa usafiri wa basi la Saratoga lenye namba za usajili T 221 DKB.
"Mashuhuda wa tukio wamesema kuwa kulikuwa na purukushani katika utekaji wa Nondo iliyosababisha begi lake dogo la nguo na pingu iliyobebwa na mmoja wa watekaji kudondoka.
"Katibu Mwenezi Mkoa wa Dar es Salaam,Monalisa Ndala na Ofisa wa Harakati na Matukio Taifa, Wiston Mogha, waliofika mapema kituoni huko walitambua haraka kuwa aliyetekwa ni Abdul Nondo kwa sababu walizitambua nguo zake kwenye begi lililodondoka na notebook yake," alisema Maharagande.
"Chama kinaendelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu tukio hili na kitatoa taarifa zaidi kwa umma. Katika hatua ya sasa tunamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Cammilius Wambura, kufuatilia haraka tukio hili na kuhakikisha Abdul Nondo anaachiwa huru mara moja," aliongeza.
Hata hivyo, Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe, alimtaja kwa jina mmiliki wa gari hilo linalodaiwa kutumika katika utekaji huo.
"Tunataka Abdul Nondo aachiwe huru mara moja akiwa mzima wa afya. Tafadhali sana, gari inadaiwa ‘parking’ (maegesho) na tumejua kila mahala gari hiyo inaegeshwa, mwacheni Nondo haraka iwezekanavyo," alisema.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime, katika taarifa yake kwa umma jana, alisema tayari jeshi hilo linafuatilia tukio hilo.
"Jeshi la Polisi lingependa kuujulisha umma kuwa Desemba Mosi mwaka huu, majira ya saa 11 alfajiri, katika eneo la Stendi ya Magufuli, Mbezi Louis, Dar es Salaam, kuna mtu mmoja mwanamume amekamatwa kwa nguvu na kuchukuliwa na watu waliokuwa wakitumia gari lenye namba za usajili T 249 CMV aina ya Landcruser rangi nyeupe.
"Ilielezwa na mashuhuda kuwa katika purukushani za ukamataji, begi dogo lilidondoshwa na baadhi ya vitu vilivyokuwamo vimetambuliwa ni vya Abdul Omary Nondo.
"Ufutiliaji wa tukio hilo ulianza mara tu ya kupokewa kwa taarifa hiyo polisi, sambamba na kufungua jalada," alisema DCP Misime.
Mnamo mwaka 2018, Nondo, akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alitoweka katika mazingira yenye utata, akituma ujumbe kwa baadhi ya jamaa zake, akidai alikuwa ametekwa.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilimkamata mkoani Iringa, likidai alijiteka ilhali alikuwa kwa mpenzi wake. Alifunguliwa mashtaka ya kujiteka mahakamani, lakini alishinda kesi hiyo. Hata alipokatiwa rufani mwaka 2019, alishinda tena.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, akizungumza na Nipashe jana kuhusu madai ya kutekwa kwa Nondo, alisema:
"Tunalaani vikali matukio ya utekaji yanayoendelea, tunaendelea kuwasiliana na vyombo vya usalama, matukio yote hatupati majibu, tunasikitishwa sana! Tunalaani ila tunahitaji kujipanga kama taifa, tutaendelea kutoa matamko zaidi baada ya kupata taarifa za kina."
Alisema wamekuwa wanamwambia Rais Samia Suluhu Hassan kuwa matukio ya utekaji nchini yanahitaji tume huru na watu huru kuyafuatilia kuliko hali ilivyo. Wanaomba tukio hili limguse ili aunde tume hiyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED