Samia kuunda tume mbili kuchunguza Ngorongoro

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:41 AM Dec 02 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema ataunda tume mbili kuchunguza kinachojiri Ngorongoro, hata kusababisha kuwapo malalamiko kwa wakazi wa eneo hilo.

Amesema tume moja itachunguza na kutoa mapendekezo kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa Ngorongoro na nyingine itaangalia utekelezaji zoezi zima la uhamiaji kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Rais Samia aliyasema hayo jana katika Ikulu Ndogo ya Arusha wakati akizungumza na viongozi wa kimila wa jamii ya Kimaasai (Malaigwanani) wanaoishi Ngorogoro. 

Taarifa iliyotolewa kwa umma na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais-Ikulu jana, ilieleza kuwa mkutano huo ulifanyika kwa lengo la kuwasikiliza viongozi hao kufuatia kuwapo malalamiko dhidi ya baadhi ya uamuzi wa serikali unaohusu eneo la Ngorongoro.

Rais Samia aliwahakikishia serikali itaendelea kuimarisha utendaji kazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya serikali na jamii hiyo.

Vilevile, alisisitiza ulazima wa wananchi kushirikishwa ipasavyo katika upangaji na utekelezaji miradi inayopita kwenye maeneo yao.

Rais Samia alisisitiza Tanzania ni nchi inayojivunia umoja wa kitaifa na yenye serikali inayowahudumia Watanzania wote. Hivyo, akaitaka Ofisi ya Rais - TAMISEMI kushughulikia changamoto zinazojitokeza ikiwamo kukosekana baadhi ya huduma za msingi za kijamii katika eneo la  Ngorongoro.

THRDC, LHRC

"Tunapongeza kwa hatua ya kukutana na watu wa Ngorongoro, imekuwa ni kilio cha muda mrefu, tumesisitiza akaonane na watu wake, huenda angekutana nao mapema zaidi yaliyotokea yasingetokea hivyo, ila tunashukuru angalau amekutana nao," alisema Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (THRDC), Dk. Anna Henga, alisema kuunda tume si kitu cha kushangiliwa sana, bali ni matokeo ya tume kuwa wazi na kufanyiwa kazi. Alitahadharisha kuwa tume nyingi zinaundwa na zinatoa mapendekezo, lakini hayafanyiwi kazi.

"Sifurahii sana tume ikiundwa, ninaona ni kunyamazishwa, huwa sioni matokeo ya tume hizi. Ngorongoro kuna changamoto kubwa, kama kweli watafanya kazi watakuja na mapendekezo yanayotekelezeka kabisa," alisema.