BAADA ya ushindi wa bao 1-0 iliyoupata Ijumaa dhidi ya Fountain Gate, Ofisa Habari wa JKT Tanzania, Masau Bwire, ametamba kuwa timu hiyo imerejea rasmi Ligi Kuu kwa ajili ya kazi moja tu ya kugawa dozi kwa kila timu itakayokutana nayo.
Akizungumza juzi akiwa Babati mkoani Manyara, Masau alisema wachezaji wao walikuwa 'wamemisi' mikiki ya ligi, na sasa wamerejea tena kwa nguvu na ari mpya, huku wakipata ushindi wa pili mfululizo.
Timu hiyo ilikuwa inacheza mchezo wa pili, baada ya kukaa nje kwa siku 29 kutokana na wachezaji wake kupata ajali baada ya basi la timu hiyo kupinduka lilipokuwa likitoka jijini Dodoma, kucheza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara, dhidi ya Dodoma Jiji, kwenye Uwanja wa Jamhuri, Oktoba 26, mwaka huu, na kujeruhi wachezaji 11.
Baada ya ajali hiyo, Bodi ya Ligi iliahirisha michezo kadhaa ya timu hiyo, ambapo ilirejea dimbani, Novemba 24, mwaka huu, ilipocheza dhidi ya Prisons na kushinda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ikishinda mchezo wa pili mfululizo Ijumaa iliyopita dhidi ya Fountain Gate, ikiwa ugenini, Uwanja wa Tanzania Kwaraa, Babati, Manyara.
"Tumerejea kwenye Ligi Kuu, hii ni mechi ya pili mfululizo tunashinda tangu kuanza tena michezo yetu, nizitahadharishe tu timu zilizobaki kuwa JKT Tanzania tumerejea kwa ajili ya kutoa dozi, tumeanza na Prisons, halafu Fountain Gate, bado wengine wajiandae," alitamba.
JKT Tanzania inatarajia kucheza mechi yake ijayo dhidi ya Pamba Jiji, Desemba 11, mwaka huu, Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ahmad Ally, aliwashukuru wachezaji wake, akisema pamoja na misukosuko waliyoipata, lakini bado wameendelea kuwa watulivu na wasikivu wakati wa mafundisho yake, kwani wanachokitoa uwanjani ndicho alichokuwa akiwafundisha kwenye uwanja wa mazoezi.
Timu hiyo ipo kwenye nafasi ya nane ya msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 16, ikicheza mechi 11 hadi sasa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED