Wananchi wa Kijiji cha Keichuru kilichopo katika Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani wamempongeza na kumshukuru Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kwa utekelezwaji wa miradi ya kupeleka umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Wametoa pongezi hizo leo wakati wa ziara ya Bodi ya Nishati Vijijini (REB) kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa kupeleka umeme katika vijiji vivyopo katika Delta wilayani Kibiti.
“Kwanza tutoe shukrani kwa taasisi zote zilizowezesha umeme kufika hapa kijijini kwetu na pongezi na shukrani nyingi kwa mama yetu Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowezesha hata sisi kufikiwa na umeme. Hata wazazi wetu wangekuja wangeshangaa sana,” amesema Mzee Hassan Malinda.
Naye Mama Anna Hamis amesema kuwa hawakutegemea umeme utafika katika kijiji chao licha ya kuwa kipo katika eneo la Delta kikiwa kimezungukwa na maji.
Mzee Iddi Ali ameshuru kwa kijiji chao kufikishiwa umeme na kusema kuwa na wao sasa wanaona matunda ya uhuru na kuhamasisha vijana kutumia umeme huo kujiletea maendeleo.
Awali akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Balozi Radhiya Msuya amesewahamashisha wananchi hao waanze kufunya maandalizi katika nyumba zao kwa kusambaza nyaya ndani ya nyumba ili umeme huo utakapowashwa waweze kuunga.
“Mhe. Rais anahaingaika usiku na mchana kutafuta fedha kwa ajili ya maendeleo yetu. Na namna pekee ya kumshukuru kwa kile anachofanya ni kuunganisha nyumba zetu na umeme huu pamoja na kutumia umeme huu kwa shughuli za maendeleo na kukuza uchumi wetu wa mtu mmoja mmoja na jamii zetu kwa ujumla,” amesema Balozi Msuya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amewataka wananchi hao kutunza na kuwa walinzi wa miundombinu ya umeme kama nyaya, nguzo na mashine umba (transfoma) kwa sababu serikali imetumia gharama kubwa kufikisha miundombinu hiyo.
“Zaidi ya Shilingi Bilioni 3.8 zimetumika kufika umeme katika vijiji hivi vilivyopo katika Delta katika Wilaya hii. Ni muhimu sana sisi tukawa walinzi wa miundombinu hii,” amesisitiza Mhandisi Saidy.
Mbunge wa Jimbo la Kibiti, Twaha Mpembenwe amemshukuru Rais kwa miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika Jimbo lake hasa miradi ya umeme vijijini na kuahidi kuwa yeye pamoja na wananchi katika jimbo hilo watakuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu ya umeme ikiwa ni njia ya kuendelea kuthamini mchango wa Serikali katika kuwaletea maendeleo.
Augustino Kiwia ambaye ni Mwakilishi wa Mkandarasi anayetekeleza mradi huo ambao ni Kampuni ya CRCEBG, amesema kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni kukatika kwa daraja na hivyo kushindwa kusafirisha nguzo za zege kwa njia ya mitumbwi. Ameahidi kuwa, pindi daraja hilo litakapokuwa limejengwa wataharakisha kazi hiyo ikamilike kwa wakati.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED