Mahakama za Tanzania zapiga hatua matumizi ya TEHAMA – Jaji Kahyoza

By Allan Isack , Nipashe
Published at 06:31 PM Dec 02 2024
RAIS wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), John Kahyoza.
Picha: Mpigapicha Wetu
RAIS wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), John Kahyoza.

RAIS wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), John Kahyoza, amesema Mahakama za Tanzania zimepiga hatua katika usikilizaji wa kesi na utoaji wa hukumu kwa wakati kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo yamechangia kuwapo kwa maboresho kwenye Mahakama hizo.

Kahyoza ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara,alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na maandalizi ya Kongamano na Mkutano wa 21 wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashari (EAMJA),unaofanyika jijini Arusha kuanzia Disemba 2 hadi 7 mwaka huu.

Ufunguzi wa mkutano wa EAMJA utafunguliwa leo(kesho), na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye atakuwa mgeni rasmi.

Hata hivyo,Jaji Kahyoza,alisema TEHAMA imesaidia kurahisisha ufunguaji wa kesi kwa njia ya mtandao,kuendesha  mashauri kwa njia ya mtandao,kupunguza muda wa mashauri kuwa Mahakamani na kupunguza viashiria vya rushwa.

Kadhalika alisema mfumo huo,umewasaidia Majaji na Mahakimu kutoa hukumu kwa haraka na kwa wakati ukilingalisha na ilivyokuwa huko nyuma sambamba na nakala za hukumu kupatikana kwa urahisi kwa njia ya mtandao.

Vilevile alisema kutokana na maboresho yaliyofanyika katika Mahakama za Tanzania nchi imefaidika kwa kuwa migogoro au kesi zinatatuliwa kwa wakati na wananchi wanakwenda kuendelea na shughuliza uzalishaji mali.

“Hatuwezi kuzuia migogoro isitokee ila inapotokea inatatuliwa kwa haraka ili wananchi wakaendelee na shughuli za uzalishaji mali kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi na familia zao,”alisema Jaji Kahyoza.

Licha ya kuzungumza hayo,alisema zaidi ya washiriki 392 watashiriki katika kongamano na mkutano mkuu na tayari wageni wameshawasili jijini hapa na maandalizi yamekamilika.

Alisema washiriki wanatoka katika nchi za Tanzania Bara,Uganda,Kenya,Rwanda,Burundi,Sudani ya Kusini na Zanzibar.