Mkoa wa Pwani umeandaa maonyesho ya nne ya bidhaa za viwandani, ambayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia Desemba 16 hadi 20, 2024, katika viwanja vya Mailimoja, Mjini Kibaha.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema kuwa washiriki 550, wakiwemo wawekezaji wa viwanda, wanatarajiwa kushiriki katika maonyesho hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha, Kunenge amesema kwamba maonyesho hayo ni njia moja ya kutafsiri kwa vitendo jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya viwanda na uwekezaji nchini.
Aidha, amesema kuwa maonyesho hayo ni fursa nzuri kwa wananchi kujionea bidhaa zinazozalishwa nchini pamoja na kujifunza teknolojia mbalimbali zinazotumika katika sekta ya viwanda.
“Tunatarajia watu 25,000 watatembelea maonyesho haya na kupata nafasi ya kuona bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi pamoja na kujifunza teknolojia mbalimbali zinazotumika katika viwanda,” amesema Kunenge.
Maonyesho hayo, yatakayofunguliwa rasmi Desemba 17, 2024, pia yatakuwa na kongamano la biashara litakalofanyika Desemba 18, 2024, katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Kwamfipa, Kibaha.
Kongamano hilo litajumuisha watendaji wa serikali, wamiliki wa viwanda, wananchi, na taasisi mbalimbali. Wataalamu wabobezi wa biashara watakuwepo kutoa mada na kujadili masuala muhimu ya biashara na viwanda.
“Niwaalike wananchi wa ndani na nje ya Mkoa wa Pwani kujitokeza kushiriki katika maonyesho haya na kongamano hili, ambapo watajifunza mengi kuhusu maendeleo ya viwanda na biashara nchini,” amesisitiza Kunenge.
Kwa sasa, Mkoa wa Pwani una viwanda 1,553, huku viwanda vikubwa 78 vikiwa vimejengwa chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan katika awamu ya sita.
Maonyesho ya viwanda katika mkoa huu yalifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2018, 2019, na ya mwisho yalifanyika mwaka 2022 mjini Kibaha. Maonyesho haya yamekuwa sehemu muhimu ya kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED