Viongozi wa dini Arusha wapongeza INEC kwa elimu uboreshaji wa Daftari la Mpiga Kura

By Allan Isack , Nipashe
Published at 06:41 PM Dec 02 2024
Msemaji wa Taasisi ya Kidini ya Kiislamu ya Twariqa Qadiriya Razikia Jailania Tanzania,Sheikh Haruna Hussein.
Picha:Mpigapicha Wetu
Msemaji wa Taasisi ya Kidini ya Kiislamu ya Twariqa Qadiriya Razikia Jailania Tanzania,Sheikh Haruna Hussein.

VIONGOZI wa dini mkoani Arusha,wameridhishwa namna Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini(INEC),inavyoshirikisha makundi mbalimbali kwa kuyaelimisha na kupokea maoni ya uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura awamu ya kwanza zoezi litakaloanza Disemba 11 hadi 17 mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Msemaji wa Taasisi ya Kidini ya Kiislamu ya Twariqa Qadiriya Razikia Jailania Tanzania,Sheikh Haruna Hussein,wakazi akizungumza na waandishi wa habari jiji Arusha kuhusu zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Sheikh Haruna,ametumia nafasi hiyo, kuwaomba viongozi wa dini,wanasiasa na viongozi wa mila kuwahamasisha wananchi kwenda kuboresha taarifa zao kwenye daftari hilo, ili wapate fursa ya kuwachagua viongozi wao mwaka 2025 kwenye uchaguzi wa Madiwani,Wabunge na Rais.

Pia kiongozi huyo wa dini,ameiomba INEC kuendelea kutoa elimu hiyo kwa uwazi hasa katika maeneo ya vijijini ambayo yamekuwa hayafikiwi kwa urahisi na wahusika waliopewa jukumu hilo.

“Naomba wananchi mjitokeze kuboresha taarifa zenu hasa kwa waliohama kutoka eneo moja kwenda eneo lingine,waliopoteza vitambulisho vyao vya mpiga kura au waliotimiza umri wa miaka 18 wakajiandikishe ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaowataka,”alisema Sheikh Haruna.

Vilevile INEC kuwawekea mazingira mazuri makundi ya walemavu na wajawazito wakati wa uboreshaji wa daftari hilo shughuli itakayofanyika kwa siku saba.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Moravian,Yohane Parkipumi, amemuomba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuendelea kuilinda na kudumisha Amani iliyoasisiwa na watangulizi wake.

Katika hatua nyingine,Mchungaji wa Kanisa hilo,amewaomba wachungazji wenzake,masheikh na viongozi wa mila kuendelea kuliombea Taifa hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwakani.