VYAMA vitano vya upinzani mkoani Shinyanga,vimeeleza kuridhishwa na uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27 mwaka huu,huku zikiomba dosari ndogondogo ambazo zilijitokeza, kwamba zisijitokeze kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Vyama hivyo ni CUF, Demokrasia Makini,NRA,CHAUMA pamoja na SAU.
Viongozi wa vyama hivyo wamebainisha hayo leo Desemba 02,2024 wakati wakizungumza na vyombo vya habari kutoa tathimini juu ya uchaguzi huo.
Wamesema uchaguzi huo umefanyika vizuri kwa amani na hapakutokea vurugu zozote, isipokuwa uligubikwa na dosari ndogondogo,ikiwamo baadhi ya watu ambao sio waaminifu kuiba kura,pamoja na kukosekana majina kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura,na kuomba Uchaguzi Mkuu 2025 zisijitokeze dosari hizo.
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi (CHAUMA) Mkoa wa Shinyanga Rashidi Katabanya, amesema uchaguzi umefanyika kwa amani na ulikuwa mzuri, isipokuwa hizo dosari ndogondogo, na kuiomba serikali katika uchaguzi mkuu mwakani (2025) ijipange vizuri ili uwe huru na haki.
Naye Grace Mnyasi Katibu wa Chama cha Demokrasia Makini mkoani Shinyanga, amesema licha ya uchaguzi huo kugubikwa na dosari ndogo ndogo, lakini ulizingatia demokrasia na kuipongeza Tume ya Uchaguzi kwa maandalizi mazuri.
Aidha,katika uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa uliofanyika novemba 27,2024, Chama cha Mapinduzi (CCM) kiliibuka na ushindi kwa kupata viti vingi, tofauti na wapinzani ambao waliambuliwa viti vichache.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED