Kiboko auawa, wananchi wagawiwa nyama

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:31 PM Nov 04 2024
Wananchi wakifurahia kumwona kiboko aliyekuwa anakula mazao yao katika kijiji cha Ilungu, wilayani Magu jana.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Wananchi wakifurahia kumwona kiboko aliyekuwa anakula mazao yao katika kijiji cha Ilungu, wilayani Magu jana.

KIBOKO aliyehatarisha maisha ya watu katika kijiji cha Ilungu, kata ya Nyigogo, wilayani Magu, ameuawa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) baada ya kuvamia mashamba ya wakulima wanaofanya shughuli za kilimo cha mpunga na mahindi katika kitongoji cha Moa, wilayani humo.

Tukio hilo lilitokea jana baada ya wananchi hao wanaolima kando ya Ziwa Victoria kushindwa kumdhibiti kiboko huyo na hivyo kuomba msaada TAWA ambao walifanikiwa kumuua kwa kumpiga risasi. Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya Ofisa Mifugo wa Kata ya Nyigogo, Hamis Gido kudhibitisha kuwa nyama hiyo ni salama kwa matumizi ya binadamu, baadhi ya wananchi walishukuru serikali kwa kuwatatulia changamoto hiyo.

Walisema eneo hilo pamekuwapo na usumbufu wa kiboko mara kwa mara lakini sasa kutokana na kiboko huyo mmoja kuuawa wanaamini hata wengine waliokuwa karibu watakimbia. Mmoja wa wananchi hao, Pungwe Wilson ambaye pia ni mkulima, alisema kuwa kwa muda mrefu pamekuwa na kilio cha wananchi kuhusu wanyama waharibifu wanaotokea ziwani.

 “Lakini sasa tunashukuru serikali kwa kumuua mnyama huyu ambaye pia amekuwa hatari hata kwa maisha yetu sisi wakulima,” alisema Wilson na kuungwa mkano na wananchi wengine, wakiwamo Magina Mbute na Ngubi Mega. 

Awali Askari wa Uhifadhi Mwandamizi kutoka TAWA, Loiruck Moses alisema wamefanikiwa kukabiliana na mnyama huyo ikiwa ni zoezi endelevu la kuwadhibiti wanyama waharibifu. Alitoa wito kwa wananchi pindi wanapokabiliana na wanyamapori wanapoonekana mahali popote, watoe taarifa ili askari wafike kukabiliana na wanyama hao. 

Ofisa Mifugo wa Kata ya Nyigogo, Hamisa Gido alisema ni suala lililozoeleka katika maeneo mengi pindi mnyama kiboko anapouawa na nyama yake kupimwa na kuonekana haina dosari yoyote, hugawiwa kwa wananchi ili wapate kitoweo. Mhifadhi Wanyamapori Wilaya ya Magu, Christopher Christian alisema wanyamapori hao wamekuwa wasumbufu kwa wananchi wa kijiji hiyo lakini wanashukuru TAWA kwa kushirikiana pamoja kudhibiti mnyama huyo.