KAMPUNI ya GOPAInfra ya nchini Ujerumani,ikishirikiana na Kampuni ya Superlit Consulting Ltd ya Tanzania,wamesaini Mkataba na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), wa kuijengea uwezo mamlaka hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake ya uboreshaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wananchi.
Mkataba huo umesainiwa leo Novemba 4,2024 katika ofisi za SHUWASA.
Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya GOPAInfra Stefan Doerner, akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, amesema Mkataba huo wa kuijengea uwezo SHUWASA, utatekelezwa ndani ya miaka minne,kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wananchi wa Shinyanga.
Naye Mkurugezi wa Kampuni ya Superlit Consulting LTD Mhandisi Fortunatus Kasimbi, ambao watafanya kazi na Kampuni hiyo ya GOPAInfra katika kuijengea uwezo SHUWASA, amesema Mkataba huo utaimarisha shughuli za Mamlaka hiyo na kufanyika kwa usahihi na ubora unaotakiwa kwa kuangalia mapungufu yaliyopo.
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA Mhandisi Yusup Katopola akizungumza kwenye hafla hiyo ya utiaji saini, amesema Mkataba huo ni sehemu mojawapo ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga, ambao unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wenye thamani ya Euro Milioni 76.
“Mkataba huu utatekelezwa ndani ya miaka minne, kuanzia leo terehe 14,2024 hadi Novemba 2028, na utakuwa msaada mkubwa sana kwetu sisi SHUWASA, na kutoa huduma bora kwa wananchi”amesema Mhandisi Katopola.
Amesema pia katika utekelezaji wa Mkataba huo, watafanya kazi kwa ushirikiano na Kampuni hizo, kwa kuhakikisha malengo ya Serikali ya uboreshaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwenye maeneo ambayo yanahudumiwa na SHUWASA, ambayo ni Manispaa ya Shinyanga,Tinde na Iselamagazi, kwamba yanakuwa na huduma bora.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED