CHADEMA Shinyanga wahofia bao la mkono uchaguzi serikali za mitaa

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 07:49 PM Nov 04 2024
Mwenyeki wa Chadema Mkoa wa Shinyanga Emmanuel Ntobi akizungumza kwenye kikao
Picha: Marco Maduhu
Mwenyeki wa Chadema Mkoa wa Shinyanga Emmanuel Ntobi akizungumza kwenye kikao

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Shinyanga,wameanza kuhofia kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao utafanyika Novemba 27 mwaka huu,watafanyiwa figisu ili wagombea wao wasishinde kwenye uchaguzi huo (bao la mkono)ili wagombea wa CCM wapate kushinda kirahisi.

Wamesema chama hicho kimekuwa hakishirikishwi kwenye masuala mbalimbali ya uchaguzi, pamoja na wagombea wao wakishindwa kurejesha fomu, kwa madai ya ofisi za watendaji kufungwa,huku wakilalamikia pia kutopewa barua ya kushiriki kuunda kamati za rufani kwenye kata, za uteuzi wa wagombea.


Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Shinyanga Emmanuel Ntobi, amebainisha hayo leo Novemba 4,2024, kwenye kikao cha kufanya tathimini ya uchaguzi ndani ya chama, na msimamo wa uchaguzi wa serikali za mitaa ambao utafanyika Novemba 27 mwaka huu.


Amesema chama hicho kwenye uchaguzi wa mwaka huu wa serikali za mitaa, kimeanza kufanyiwa mizengwe mbalimbali, pamoja na wagombea wao kuanza kutishwa,kufungiwa ofisi ili wasirudishe fomu, na pia kutoshirikishwa kwenye masuala mbalimbali ya uchaguzi, ili wagombea wao wakose sifa na kuenguliwa kushiriki kwenye uchaguzi huo.
 

“Uchaguzi wa mwaka huu wa serikali za mitaa Chadema Shinyanga tumeanza kufanyiwa mizengwe, ukiangalia ratiba ya Tume leo tarehe 4 ilikuwa ni siku ya uteuzi ya kamati za rufani kwenye Kata zetu, na kwenye kamati hiyo lazima aingie mwanasiasa wa chama chochote, lakini mpaka navyoongea muda huu CHADEMA hatujaona barua yoyote ya kuitwa kushiriki kuunda kamati ya rufani, hivyo umma unapaswa kujua namna bao la mkono linavyotengenezwa,”amesema Ntobi.


Aidha,ametoa rai pia kwa Tume ya Uchaguzi, kwamba kwa kuzingatia 4R za Rais Samia na Katiba ya nchi ya mwaka 1977 ibara 3, kuwa Tanzania ni nchi ambayo inaheshimu misingi na demokrasia, kuwa hawategemei wagombea wao kuenguliwa kugombea kwenye uchaguzi huo,na kutoa tahadhari kama wanalipenda taifa na kufuata misingi ya haki na demokrasia wasiengue wagombea wa CHADEMA siku ya Novemba 8.


Wameviomba pia vyombo vya ulinzi  kuwa linda wagombea wao wa CHADEMA ili wawe salama, kutokana na baadhi yao wameanza kupokea vitisho, ili wajiondoe kushiriki kugombea  kwenye uchaguzi wa serikal za mitaa.


“CHADEMA kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa,tunataka uwe huru,haki uwazi na ukweli, na sisi tutakuwa wa kwanza kukubali matokea endapo tumeshindwa kwa haki,na tunatoa Rai kwa CCM na dola na wao wakubali matokeo pale mgombea wa Chadema akishinda, na hiyo ndiyo maana ya demokrasia,”amesema Ntobi.

 
Katika hatua nyingine, amesema siku ya kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa novemba 27, kwamba kutatokea mgogoro mkubwa, wakidai kwamba baadhi ya maeneo wameandikishwa wanafunzi ambao siyo wakazi wa eneo husika, na kwamba katika uchaguzi huo wamejipanga vyema kulinda kura zao.


Naye Afisa wa Organization,mipango na uchaguzi Kanda ya Serengeti kutoka CHADEMA, Joseph Ndatala, amesema kwenye uchaguzi huo wa serikali za mitaa, kwamba wapo imara na hakuna Mgombea wao ambaye ataenguliwa jina lake.