KAMBI ya Madaktari Bingwa wa Mama Samia, wamewasili mkoani Shinyanga kwa awamu nyingine tena, kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi.
Kambi hiyo imewasili leo Novemba 4,2024 mkoani Shinyanga, na kupokelewa na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,na kisha madaktari hao kusambaa katika halmashauri zote sita za mkoa huo.
Mratibu wa Madaktari hao Bingwa wa Mama Samia Everine Maziku kutoka Wizara ya Afya,idara ya Mama na Mtoto, amesema Madaktari hao bingwa wapo 47, ambapo watawafikia wananchi katika maeneo yao na kupata matibabu ya kibingwa.
“Tunampongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kampeni hii ya Madaktari bingwa, ambayo imekuwa ikisaidia wananchi wasio na uwezo kupata matibabu ya kibingwa huko huko katika maeneo yao na kuokoa afya zao,”amesema Everine.
Aidha, amesema mbali na madaktari hao kutoa matibabu ya kibingwa kwa wananchi, pia watawajengea uwezo watoa huduma kwenye hospitali ambazo watakuwa wakitibu wananchi, pamoja na kuanzisha huduma zingine ambazo hazikuwepo kwenye hospitali hizo.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Faustine Mlyutu, amesema madaktari hao watakuwa mkoani Shinyanga kwa muda wa siku Sita katika halmashauri zote za mkoa huo, huku akiwasisitiza Waganga Wakuu wa Halmashauri, kwamba waendelee kufanya kampeni ya kuhamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kupata matibabu ya kibingwa.
“Wananchi wa Shinyanga nawaomba wajitokeze kwa wingi kupata matibabu ya kibingwa kutoka kwa Madaktari hawa bingwa wa Mama Samia na kuokoa afya zao,”amesema Mlyutu.
Baadhi ya Madaktari hao bingwa akiwamo Missano Yango kutoka Hospitali ya Rufaa Dodoma, ambaye ni bingwa wa Magonjwa ya nje, amesema wamejipanga vyema kutoa huduma stahiki za matibabu kwa wananchi na kuwasihi wajitokeze kwa wingi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED