Mende ajitokeza kugombea TUCTA

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 08:07 PM Nov 04 2024
Mtumishi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Eben-Ezery Mende
Picha: Grace Gurisha
Mtumishi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Eben-Ezery Mende

Mtumishi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Eben-Ezery Mende amejitokeza kugombea nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Akizungumza na leo Nipashe Digital jijini Dar es Salaam, Mende amesema amewiwa kuigombea nafasi hiyo kwa kuwa uongozi ni karama aliyotunukiwa na Mungu na anaamini ataitendea haki nafasi hiyo.

"Si kila mtu ana karama ya uongozi na waliopewa karama hiyo wasipoitendea kazi watadaiwa siku ya mwisho. Mungu alienipa tunu hiyo ndiye atakaehusika ndani yangu" amesema Mende.

Amesema watumishi nchini wamepungua msisimko wa kufanyakazi kwa sababu nyingi ikiwemo ya watu wanaopaswa kuamsha msisimuo huo kutulia.

Pia amesema akipata nafasi hiyo atahakikisha utaratibu wa wajibu na haki vinazingatiwa kama ilivyo utaratibu wa tamakali ya nahau hiyo.

Uchaguzi huo utafanyika jijini Dodoma Novemba 14 mwaka huu kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Cornel Maghembe aliyeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Wilaya.

Kwa mujibu wa Mende, TUCTA ni taasisi kubwa inayohitaji umakini mkubwa kiuongozi na kwa namna alivyojipima amejiridhisha kwamba ataiongoza vema na kuweka historia nzuri ya kiuongozi.

Mende amewahi kuwa kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Huduma na Ushauri (TUICO) Mkoa wa Shinyanga.