Lissu aweka msimamo upinzani kuungana 2025

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 11:38 AM Nov 04 2024
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tanzania Bara, Tundu Lissu.
Picha: Mtandao
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tanzania Bara, Tundu Lissu.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tanzania Bara, Tundu Lissu amesema mpango wa vyama vya upinzani kushirikiana katika baadhi ya maeneo wakati wa uchaguzi kwa ajili ya kuweka nguvu zaidi ya ushindi ni jambo jema.

Hata hivyo, mtaalamu huyo wa sheria amesema tatizo kubwa linalochangia jambo hilo lisiwezekane ni kwamba vyama vyenye uwezo wa kuweka wagombea havifiki hata vinne.

Lissu amesema jana kuwa vyama vingi vya upinzani nchini havina uwezo wa kusimamisha wagombea au kufanya kampeni na kwamba hata takwimu katika uchaguzi uliopita zinaonesha havifikishi asilimia tano ya kura za wabunge na asilimia tatu ya kura za Rais huku vyama vinavyofanikiwa kusimamisha wagombea maeneo mengi ya nchi vikionekana ni viwili tu -- Chama Cha Mapinduzi (CCM) na CHADEMA.

Ni kauli aliyoitoa mwishoni mwa wiki wakati wa mahojiano kwenye kipindi cha Medani za Siasa kinachorushwa na Star Tv.

"Tuzungumze ukweli; maeneo ya kuunganisha nguvu ni machache sana, sehemu kubwa ya vyama katika nchi hii, ni CCM na CHADEMA. Sasa huko ambako viko vyama hivyo viwili ukisema tuunganishe, tunaunganisha nguvu na nani ambaye hatumwoni kabisa? Hawapo kabisa hata kwenye mikutano, hawapo kwenye uchaguzi... tuunganishe nguvu kwa sifuri, ukijumlisha sifuri sawa na sifuri. 

"Kama vyama vya upinzani vipo na vimejipanga kuangalia maeneo ya kuunganisha nguvu kwenye chaguzi si jambo baya, tatizo ni kwamba vyama vya upinzani vyenye uwezo wa kuweka wagombea kwenye uchaguzi wowote ule katika nchi yetu ni vingapi hasa?" Lissu alihoji.

Alisema vyama vya siasa vilivyoandikishwa vipo zaidi ya 20, lakini ambavyo huwa vinaweka wagombea havifiki vinne.

"Una uhakikia CCM itaweka wagombea? Una uhakika CHADEMA itaweka wagombea kila mahali? Utakuwa na uhakika kwamba ACT-Wazalendo itaweka wagombea wote wanaohusika Zanzibar lakini baada ya hapo vyama vingine viko wapi?

"Ukitaka kujua nani ni nani katika uchaguzi wa Tanzania, angalia takwimu zozote za uchaguzi wetu. Pamoja na matatizo yote ya uchaguzi wetu, angalia takwimu za huo uchaguzi. Hivyo vyama vingine vyote, 2020 ukiondoa CCM na CHADEMA, havikufikisha asilimia tano ya kura za wabunge, havikufikisha asilimia tatu ya kura za Rais.

"Haviweki wagombea, havifanyi kampeni, vyama vingine hivi vinaishi katika madaftari ya Jaji Fransis Mtungi tu (Msajili wa Vyama vya Siasa nchini). 

"Huko utavikuta lakini ukija huku waliko wananchi unakutana na viwili, vitatu, ukienda mikoani ni viwili, vitatu... ukienda kwa msajili wanakuambia aah... tuna vyama 23. Tuna tofauti ya vyama vilivyopo katika madaftari ya Jaji Mtungi na vyama ambavyo viko mtaani na vijijini katika nchi yetu," alisema Lissu.

Mwanasiasa huyo pia alitoa maoni yake kuhusu kuondolewa kwa Rigathi Gachagua katika kiti cha Naibu Rais wa Kenya, akisema hilo limetokana na mfumo wa uchaguzi na kikatiba wa nchi hiyo ambao Tanzania ina jambo la kujifunza kwake.

"Kwangu mimi ule utaratibu wa kumwondoa madarakani Naibu Rais wa Kenya, unathibitisha ushindi wa demokrasia ya nchi hiyo, unathibitisha ushindi wa mfumo wa kikatiba wa nchi hiyo ambayo imeweka utaratibu wa kumwondoa Makamu wa Rais madarakani na Rais mwenyewe kama ikionekana kwamba amefanya vitendo vinavyopingana au kukiuka katiba ya nchi yao.

"Wanachofanya Wakenya wanathibitisha ukuu wa katiba na misingi yake imara na misingi imara ya taasisi zao za dola pamoja na mambo makubwa kama hayo yanafanyika hadharani, bungeni waziwazi, mbele ya wananchi na uamuzi unafanywa na vyombo vyenye mamlaka ya kuamua kwa njia za kikatiba.