Ni zama za mabadiliko Wamasai wanapogeuka wakulima mahiri

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 09:19 AM Nov 05 2024

Mkulima Mathayo Olonyoke, akiwa kazini kwenye shamba alilootesha mikunde.
PICHA: MAULID MMBAGA
Mkulima Mathayo Olonyoke, akiwa kazini kwenye shamba alilootesha mikunde.

NI kwa nadra kumkuta Mmasai njiani na jembe begani akielekea shambani. Tena si kawaida kuwaona wameinama wanalima, japo kuna baadhi ya jamii za Wamasai wanaojulikana kama Wakwavi ambao hufuga na kwa kiasi wanalima.

Leo, zama zimebadilika baada ya wadau wa kilimo kuibua mikakati ya kuhamasisha na kubadilisha jamii hiyo na sasa inaingia mashambani kuzalisha mazao.

Ni jitihada ambazo Taasisi ya Uendeshaji wa Mifumo ya Masoko ya Kilimo (AMDT), imekuwa ikizifanya kwa miaka kadhaa ikiwamo kutoa elimu na kujenga miundombinu ya umwagiliaji ambazo zimebadili mtazamo wa wafugaji hao na kujikita katika uzalishaji.

Ofisa Kilimo wa Kata ya Ondonyongijape wilayani Simanjiro mkoani Manyara, ambako idadi kubwa ya wananchi ni Wamasai, Jenifa Mbuya, anasema  eneo hilo takribani asilimia 99 wakazi wake ni wakulima.

Anasema wale walioanza kulima mwanzoni wamekuwa sehemu ya kuwashawishi wanaotegemea ufugaji pekee kubadilika, akieleza kuwa wakulima wamekua na chakula cha uhakika na familia hazina njaa.

 “Waliokuwa wa kwanza kulima akipata changamoto anauza gunia la maharage na kujihudumia, hauzi mifugo hivyo aliongeza ng’ombe huku ikitatua matatizo mengine na kuona kuwa kilimo ni tija.

“Waliokuwa wanasema Wamasai hawalimi sio wa Simanjiro. Leo asilimia kubwa wameingia kwenye kilimo, kwa kushirikiana na AMDT tuliweka mashamba darasa wamependa na  kujiendeleza,” anasema Jenifa.

Kwa takwimu za awali inaelezwa kuwa jitihada hizo zimekuwa na matokeo chanya kiasi cha kuwafanya wafugaji kuona kwamba kilimo na ufugaji vyote vina thamani sawa.

Mathayo Olonyoke, mkazi wa Kijiji cha Orkirung’urung’u, Simanjiro, mfugaji wa jamii ya Kimaasai, anasema alianza kulima baada ya kuibuka changamoto za mabadiliko ya tabianchi ziliathiri ufugaji.

Anasema wakiwa katika harakati za kutafuta mbadala wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi AMDT iliwapatia elimu ya namna ya kufanya kilimo cha kisasa.

Anabainisha kuwa ni miaka 20 sasa tangu aanze kulima na kwamba baada ya kupatiwa elimu na taasisi hiyo ikishirikiana na kampuni ya mbolea ya Beula kuhusu kilimo cha umwagiliaji wa matone, amezidi kupata mafanikio yanayochochea hamasa kwa jamii hiyo.

“Nawaambia wafugaji na Wamasai wenzangu kwamba kilimo ni kizuri na kinasaidia kupiga hatua kimaisha. Ingawa kuna changamoto lakini hata kwenye ufugaji ziko pia, lakini kutokana na hatua niliyoipiga hata nikiwaambia wafugaji tulime inakuwa rahisi kunielewa kwasababu kila kitu wanakiona,” anasema Olonyoke.

Anasema kupitia mradi wa maono ya mabadiliko kwenye mazao na udongo (VACS), unaoendeshwa na AMDT, wananufaika na mbegu bora na kuhamasishwa kulima choroko na kunde zinazovumilia ukame.

Anafafanua kuwa kilimo hicho kimekuwa na uhakika wa chakula muda wote, akieleza kwamba kabla hawajafikiwa na mradi huo wa umwagiliaji hawakuwahi kupata mboga za maharage katikati ya msimu au kwenye kiangazi.

“Manufaa tunayo kwasababu tukitaka mboga leo tunapata kwa wakati, binafsi najisikia vizuri na ninafikiri wafugaji wenzangu wanatamani ninachokifanya na kila siku wananipongeza na wengi wanaahidi kujiunga na mimi,” anasema Olonyoke.

Aidha, anaomba wadau mbalimbali kuwashika mkono kwa kuwachimbia visima zaidi ili waongeze ukubwa wa mashamba kwasababu wana maeneo mengi lakini wanashindwa kuyapanua kutokana na uhaba wa maji.

KUBADILI MTAZAMO

Kuhusu migogoro ya wafugaji na wakulima Olonyoke anaeleza kuwa wanakijiji wamewekeana miongozo kwa kushirikiana na ofisa kilimo wa eneo hilo, akieleza kwa sasa imefika hatua wanaona kuwa kilimo ni bora kama ufugaji na hawataki shughuli yoyote iiathiri nyingine.

Anasema wameshapiga vita na kukemea masuala ya kudhuru ng’ombe na kwamba inapotokea mifugo imeharibu mazao, wanataka ofisa kilimo atathimini shamba kisha ichukuliwe hatua haraka mkulima alipwe fidia.

“Tunalinda sana, tumeshasema hatutegemei mifugo yenyewe, kwa hiyo kilimo ni uhai wetu na ni bora kama mifugo, na hatutegemei kuona ng’ombe ikienda kula shambani, na maeneo mengi tuliyolima mazao hatujaweka uzio lakini hakuna anayeweza kuthubutu kuharibu mifugo,” anasema Olonyoke.

Hata hivyo, anaeleza kuwa kilimo cha kisasa cha umwagiliaji ambacho amekuwa akijihusisha nacho kwa zaidi ya miaka 20, kimempatia mafanikio mengi ikiwamo kuchochea hali yake ya kiuchumi, uhakika wa chakula na kusomesha watoto wake ambao wako chuo kikuu.

Anasema ujuzi na zana ya kilimo anavirithisha kwa watoto wake, akieleza kuwa hakuna mtoto katika familia zao ambaye hajui kulima.

“Ninavyo vifaa mbalimbali kama trekta na vijana wangu wanaoendesha, wanalima wanaotesha wenyewe, wanapalilia na wanafanya kila kitu, hivyo inatosha kusema kwamba kwa sasa kwenye kilimo tumebobea, tunalima na kufundisha wengine,” anasema Olonyoke.

Baraka Mathayo, ni mtoto wa Olonyoke, anasema amemuona mzazi wake akijihusisha na kilimo kwa muda mrefu, na ndicho kilichomsomesha kuanzia ngazi ya msingi  hadi elimu ya juu akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Elimu DUCE.

Anamtaja mzazi wake kuwa ni mkulima mahiri  anayeshirikiana na wataalamu wa kilimo kama AMDT na Beula katika kumwongezea mbinu mbalimbali za kitaalamu na kulima kwa tija.

“Katika mradi huu wa umwagiliaji naona kuna mafanikio makubwa kwasababu ukiangalia shamba linapendeza muda wote, tunapata mboga na chakula kwa wakati wote hatuhitaji kununua hata maisha tunayaona ni mazuri.

Anaongeza: “Kutokana na elimu yangu, nitapambana kuendelea kuelimisha jamii yetu ya Kimasai kuhusiana na kilimo kwasababu ndicho kilichompa mzazi wangu  pembejeo kama trekta, nyumba, kuongeza miundombinu ya kilimo, kununua ardhi, pamoja na kutusomesha na wadogo zangu,” anasema Mathayo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Orkirung’urung’u, Noa Moringe, anasema miezi ya Septemba na Oktoba afya ya mifugo inadhoofika, wakati huo huo thamani ya mazao ikipanda, na kwamba hiyo ni moja ya sababu iliyowashawishi wafugaji kujihusisha na kilimo.

“Tulianza kulima lakini pia tukifuga ng’ombe mmoja hadi watatu lakini baadae tulipata faida mara dufu. Tumeona manufaa ya kilimo kwa sasa Wamasai wanalima.

“Wananchi wamepata mwamko kwenye kilimo kutokana na elimu na hamasa tuliyopatiwa na AMDT, na tunampongeza sana Olonyoke amekuwa mfano wa kuigwa katika kijiji hiki kwa kuwa ndiyo mkulima wa kwanza kujihusisha na umwagiliaji wa matone,” anasema Moringe.

MSIMAMO WA WADAU

Mkurugenzi wa AMDT, Charles Ogutu, anasema lengo la taasisi ni  kuionyesha jamii njia na kuipatia baadhi ya vitu  kuwashawishi watu kujiunga na kilimo, huku wakishirikiana na serikali ambayo inaendesha mpango wa uchimbaji visima katika maeneo mbalimbali.

Anasema wanatamani kuendelea kuona mabadiliko kwenye jamii ya wakulima, akieleza kuwa wanaamini inawezekana na kwamba wakulima wengi wanachokosa ni elimu na ushahidi wa kile wanachotakiwa kufanya.