KIUNGO wa Simba, Yusuph Kagoma, ataendelea kuwa nje ya uwanja kwa angalau wiki tatu zaidi akiendelea kupata matibabu ya jeraha lake la mguu.
Kagoma hajaonekana uwanjani tangu baada ya mchezo wa dabi ya kariakoo dhidi ya Yanga uliochezwa Oktoba 19, mwaka huu, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao hakumaliza baada ya kuumia na kutolewa nje.
Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ali, alisema nyota huyo bado yupo kwenye matibabu ya wiki tatu zaidi.
"Nyota wetu Yusuph Kagoma bado yupo kwenye matibabu, ana wiki tatu zaidi za matibabu na inshallah atarejea uwanjani kuendelea na majukumu yake," alisema Ahmed.
Alisema baada ya kupata majeraha alianza matibabu na taarifa alizonazo ni kuwa ana wiki tatu za matibabu kabla ya kuanza kurejea uwanjani.
"Wanasimba wasiwe hofu, mchezaji wetu anaendelea na matibabu, najua wengi wanatamani kumuona uwanjani, niwahakikishie atarejea hivi karibuni," aliongeza kusema Ahmed.
Kagoma tangu kutua Simba kwenye dirisha lililopita akitokea Singida Big Stars, ameonesha kiwango bora na kuwa kipenzi cha mashabiki wa klabu hiyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED