Fadlu: Dabi ijayo Simba, Yanga itaamua bingwa

By Adam Fungamwango ,, Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 10:29 AM Nov 05 2024
 Fadlu: Dabi ijayo  Simba, Yanga  itaamua bingwa
Picha: Mtandao
Fadlu: Dabi ijayo Simba, Yanga itaamua bingwa

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema anaamini kuwa dabi ya mzunguko wa pili kati ya timu yake dhidi ya Yanga ndiyo inaweza kumpata bingwa wa Tanzania Bara, hivyo hana presha na ubingwa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, kocha huyo alisema kwa sasa anachoangalia ni kuhakikisha timu yake inapata pointi tatu kwenye kila mchezo ili kufikia malengo.

Alisema anafurahishwa sana na viwango vya wachezaji wake kwa jinsi wanavyojitoa na kupambana, ingawa changamoto kubwa anaiona kwa waamuzi ambao hawawalindi kwa kuruhusu wapinzani kuwachezea vibaya hata ndani ya eneo la hatari, lakini wamekuwa wakifumba macho.

“Nafurahishwa na viwango vya wachezaji wangu, wamekuwa wakipambana, lakini nimeongea nao na kuwaeleza juu ya kucheza bila ya kukata tamaa ndani ya uwanja kwa kuwa mpira hauishi hadi filimbi ya mwamuzi inapopigwa, licha ya kwamba wanakutana na changamoto ya waamuzi ambao wamekuwa hawawalindi, wamekuwa wakichezewa vibaya na wapinzani nje na ndani ya boksi, lakini wanaangalia tu.

"Kuhusu ligi bado mbio ndefu ni mapema sana kukata tamaa kuhusu ubingwa, nadhani mzunguko wa pili tutakapomaliza dabi kila kitu kitakuwa wazi na kupata mwanga wa mbio za ubingwa,” alisema Fadlu.

Alisema kwa sasa atakuwa anafanya mabadiliko ya mfumo kulingana na mpinzani watakayekutana naye, kwani amegundua kila timu inakuja na malengo na mfumo tofauti jinsi ya kuwakabili.

"Wengine hawaji kutafuta ushindi, wanakuja kutuzuia sisi kupata ushindi," alisema.

Kuhusu mchezo dhidi ya KMC FC, utakaochezwa kesho Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam, Fadlu alisema haitokuwa rahisi, lakini pointi tatu muhimu sana kujiweka katika mazingira mazuri.

"Tuna waheshimu wapinzani wetu, tunahitaji kufanya vizuri katika mchezo wetu dhidi ya KMC mara ya mwisho tulitoka nao sare ya mabao 2-2, hatutaki kujirudia,” alisema.

Hata hivyo, Fadlu hakuwapo kwenye mchezo huo badala yake aliyekiongoza kikosi hicho wakati huo alikuwa ni Mbrazil, Roberto Oliveira Robertinho.

Fadlu aliongeza: "KMC ni timu nzuri na wapo kwenye kiwango kizuri, watakuwa kwenye uwanja wao hivyo natarajia ushindani mkubwa kutoka kwao, kama timu tumejiandaa vizuri na tunaendelea na maandalizi yetu".

Alisema kuwa baada ya safari ndefu kutoka Kigoma, walifanya mazoezi mepesi na sasa wanaendelea na maandalizi ya mchezo huo.

"Tulifanya kazi kubwa sana Kigoma, wachezaji wangu walijituma sana na tulifanikiwa kupata ushindi dhidi ya Mashujaa, baada ya hapo niliwataka wachezaji wasahau matokeo hayo na kuweka mipango yetu kwenye mchezo na KMC," alisema Fadlu.

Alisema kwenye mchezo wa kesho wataingia uwanjani wakiwa na lengo la kuondoka na pointi zote tatu, lakini hawatawadharau wapinzani wao hao.

"Nimewaangalia KMC kwenye baadhi ya michezo yao, ni timu nzuri, ni lazima wachezaji wangu wajitoe na kupambana kama walivyofanya Kigoma ili tufikie lengo letu la kuondoka na pointi zote tatu," alisema Fadlu.

Rekodi zinaonesha timu hizo zimekutana mara 12 tangu KMC ilipopanda daraja, huku takwimu zikibainisha kuwa Simba imeshinda mara 10 na sare mbili, huku timu hiyo inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni ikiwa haijawahi kupata ushindi wowote dhidi ya Wekundu wa Msimbazi hao.

Iwapo Simba itashinda mchezo wa kesho itafikisha pointi 25 na kukwea hadi kileleni mwa msimamo huku ikisubiri mchezo wa Alhamisi ijayo, ambao watani zao wa jadi, Yanga wenye pointi 22, watakapocheza dhidi ya Tabora United, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.