Kamati kuamua utata penalti iliyovunja mechi Ligi Kuu Z'bar

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 10:41 AM Nov 05 2024
Kamati kuamua utata penalti iliyovunja mechi Ligi Kuu Z'bar
Picha: Mtandao
Kamati kuamua utata penalti iliyovunja mechi Ligi Kuu Z'bar

BAADA ya mchezo wa Ligi Kuu Zanzibar kati ya Mwenge SC na Uhamiaji FC kushindwa kuendelea na kuvunjika kabla ya dakika nne za nyongeza ili kukamilisha dakika 90 za mpira kuchezwa uwanjani katika Dimba la Finya, Kisiwani Pemba juzi, maamuzi sasa yatatolewa ndani ya saa 72, imeelezwa.

Mchezo huo ambao ulichezwa mwishoni mwa wiki ulivunjika wakati timu hizo zikiwa bado hazijafungana, kutokana na Uhamiaji FC kugomea mchezo huo baada ya wapinzani wao kupewa penalti. 

Uhamiaji FC ilitoka uwanjani baada ya mwamuzi wa mchezo huo kutoa penalti kwa timu ya Mwenge SC tukio lililolalamikiwa na benchi la ufundi lao na kuamua kutoka nje ya uwanja, hivyo mechi kuvunjika.

Akithibitisha juu ya tukio hilo lililotokea Finya Kisiwani Pemba, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Shirikikisho la Soka Zanzibar, Issa Kassim, alisema bodi kupitia Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, itapitia ripoti ya mwamuzi juu ya mchezo huo na kutoa maamuzi.

Alisema kamati hiyo itakutana ndani ya saa 72 ili kuhakikisha inatoa maamuzi hayo kwa haraka kabla ya kuanza mzunguko wa 10 wa ligi hiyo.

“Maamuzi yatotoka haraka ndani ya muda wa saa 72 kama inavyosema kanuni, na kitendo kilichofanyika kwa ngazi hii ya Ligi Kuu si kizuri na hakina afya,” alisema.

Aidha, alisema Bodi ya Ligi imewataka viongozi wa klabu kupitia mabenchi yao ya ufundi kuzingatia nidhamu mchezoni pamoja na kuzisoma kanuni.

Alisema kupitia matukio ambayo yanajitokeza katika Ligi Kuu Zanzibar hasa ya kinidhamu, mengi yao yanasababishwa na mabenchi ya ufundi.

Kassimu alisema Bodi ya Ligi kwa kushirikiana na kamati ya ufundi inatarajia kufanya kikao maalum na walimu wa timu zote za Ligi Kuu katika kipindi hiki ambacho ligi hiyo inaendelea ili kuhakikisha matukio kama hayo hayajirudii tena.