Maziko ya Musuguri yawakutanisha majenerali

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:44 AM Nov 05 2024
Maziko ya Musuguri yawakutanisha majenerali
Picha: Mtandao
Maziko ya Musuguri yawakutanisha majenerali

MWILI wa Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali David Musuguri umezikwa kijijini kwao wilayani Butiama, mkoani Mara alikoishi kwa miaka 36 baada ya kutumikia jeshini kwa miaka 44.

Hatua ya kuweka mwili wake kaburini ilikuwa jana saa 6:41 mchana, kukishuhudiwa orodha ya waombolezaji inayowajumuisha Wakuu wa Majeshi wastaafu waliompokea kama vile Majenerali Robert Mboma, George Waitara na Venance Mabeyo.   

Sambamba na hilo, ni tukio lililowakusanya makamanda wa ngazi za juu mbalimbali wastaafu wa muda mrefu na mfupi, huku tukio likichukua saa kadhaa, likitawaliwa na sanaa zote za kijeshi na kiimani, likiongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma, Michael Msonganzila.

Aidha, kiongozi wa kimila aliyewakilisha kundi la maisha yake mapya ya miongo mitatu na nusu kijijini, alikuwa Chifu wa Kabila la Wazanaki, Edward Wanzagi.

Akiongoza ibada ya maziko ya mwili wa Jenerali Musuguri, Askofu Msonganzila alisema, "Ukisimuliwa vita ambavyo amevipitia ndani na nje ya nchi, mazingira ya vita ni ya kifo, kuua au kuuawa, lakini yeye alitoka mzima huko kote. 

"Kwa Kiswahili wangesema 'ana Mungu wake' kwa sababu wengi walifariki dunia, wakiwamo viongozi na askari wa kawaida."

Mtazamo huo ulitolewa tafsiri nyingine na Mkuu wa Majeshi wa sasa, Jenerali Jacob Mkunda, ambaye anakiri hakuwahi kufanya naye kazi, lakini waliomtangulia wamempa sifa nyingi ya upendo jeshini na uzalendo.

Akizungumza baada ya ibada na taratibu za mazishi, Jenerali Mkunda alisema Jenerali Musuguri atakumbukwa si ndani tu ya Tanzania, bali pia nje ya Tanzania kutokana na mambo aliyoyafanya, akilitumikia Jeshi la King’s African Rifles (KAR) pamoja na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Alisema Jenerali Musuguri katika kipindi cha miaka 104 ya maisha yake, alitumia miaka 44 na siku 24 sawa asilimia 43 ya uhai wake katika utumishi wa umma kupitia JWTZ.

“Alitumikia jeshi kwa uhodari, ushujaa, uaminifu, utiifu na uadilifu mkubwa. Jenerali Musuguri alitumikia vyema Jeshi la King’s African Rifles (KAR), alishiriki vita ya pili ya dunia chini ya majeshi ya Uingereza na washirika wake ambavyo vilimjenga, kumkomaza na kumpa uzoefu mkubwa na kuwa ‘battle harden soldier’, uzoefu aliotumia kulijenga jeshi la nchi mara na baada ya uhuru.

“Baada ya maasi ya mwaka 1964, jeshi liliundwa upya na kupatikana JWTZ ambako Jenerali Musuguri alitumikia akiwa katika vyeo na madaraka mbalimbali akiwa miongoni mwa waanzilishi wa jeshi hili kisha kupandishwa vyeo na kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi mwaka 1980 na kustaafu utumishi mwaka 1988," alisema Jenerali Mkunda.

Alisema kuwa Jenerali Musuguri ni miongoni mwa watu walioshiriki kulijenga na kuliimarisha jeshi hilo, akihudumu katika vikosi vyote vya mwanzo ambavyo ni battalion 1, 2 na 3 na baadaye kuziongoza brigedi 201 na 202 na kisha kamanda wa divisheni ya 20 ambako aliteuliwa kuwa kamanda wa operesheni katika Vita vya Kagera baada ya kukombolewa kwa ardhi ya Tanzania. Hivyo, kusimamia mipango yote ya vita hiyo. 

Maziko ya mwili wa Jenerali Musuguri yaliongozwa kiserikali na Naibu Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko na huku kukiwa na viongozi wengine wa serikali na dini kutoka ndani na nje ya nchi.

Akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika maziko hayo, Naibu Waziri Mkuu Biteko alisema taifa litaendelea kumwenzi kwa ujasili wake Jenerali Musuguri ikiwa ni pamoja na kujitoa kujiunga jeshini akiwa na umri mdogo wa miaka 22 chini ya jeshi la wakoloni.

"Alihakikisha Tanzania inabaki kuwa na amani, usalama na mshikamano, hivyo kama familia na Watanzania wote niwaase tuendelee kushikilia imani yake pamoja na maono yake hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi, tuishi bila kuharibu amani ya taifa letu," alisema Dk. Biteko.

Aliwataka wanafamilia kuendelea kuwa na mshikamano kama alivyokuwa Jenerali Musuguri na kuwa na moyo wa subira bila kukubali kufarakanishwa na mtu yeyote ili iwe sehemu ya kuenzi maisha yake.

Chifu wa Kabila la Wazanaki, Edward Wanzagi, alisema kabila hilo ndilo limemzaa na kumlea Musuguri ambaye alikuwa ni mtu muhimu mwenye kipaji, uwezo, utu, uadilifu na haiba ya kipekee.

Alisema kuwa pamoja na umaarufu wake wote, alikuwa ni mtu wa tofauti ambaye alimjali na kumthamini, kumpa heshimu na kumsaidia kila mtu kuanzia watoto, vijana na hata wazee.

Alisema Jenerali Musuguri aliwasaidia kuondokana na migogoro ya mipaka kutokana na kuyafahamu ipasavyo maeneo ya mipaka yao, hivyo kuomba mipaka hiyo iendelee kuheshimiwa.

Jenerali Musuguri alizaliwa mwaka 1920 wilayani Butiama na kujiunga na Jeshi la King’s African Rifles (KAR) mwaka 1942 ambalo alilitumikia mpaka kipindi cha maasi na kuanzishwa JWTZ mwaka 1964 kisha kuongoza Vita vya Kagera na baadaye kuteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi mwaka 1980, nafasi aliyoitumikia hadi anastaafu mwaka 1988.

Jenerali Musuguri alifariki Dunia Oktoba 29 mwaka huu katika Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando, mkoani Mwanza alikokuwa anapatiwa matibabu.

Wakuu wa majeshi nchini tangu kuundwa JWTZ ni Majenerali Mirisho Sarakikya (1964-1974), Twalipo (1974-1980), Musuguri (1980-1988), Mwita Kiaro (1988-1994), Waitara (2001-2007), Mwamunyange (2007-2017), Mabeyo (2017-2022) na wa sasa Mkunda.

*Imeandaliwa na Vitus Audax na Neema Emmanuel (MWANZA)