MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameweka wazi sababu iliyochangia kushindwa kujiandikisha katika Daftari la Wakaazi ili kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Kauli hiyo ya Lissu imekuja ikiwa ni siku chache tangu Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Amos Makalla, atamke kwamba kiongozi huyo mkuu ndani ya CHADEMA hakujiandikisha na "ameweka rekodi yake ya kiongozi wa chama kutokupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa".
"Sikujiandikisha kwenye daftari kwa sababu niliondoka Oktoba 2 kuja Ubelgiji kufuatilia mambo yangu ya kufungua kesi dhidi ya kampuni moja ya simu, nilitarajia kuwa ningerudi mapema lakini haikuwezekana, bado nipo huku," alisema Lissu.
Oktoba 22, mwaka huu, akipokea ripoti ya uandikishwaji mkoa wa Dar es Salaam, Makalla alisema alitarajia kiongozi huyo mkuu ndani ya chama chake, angeonesha mfano kwa wanachama na wafuasi wake kama ambavyo viongozi wengine wamefanya kwa kuwa mstari wa mbele kujiandikisha katika daftari hilo.
"Nionesheni mahali popote Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu alipojiandikisha. Atapataje uhalali wa kuhoji kuhusu kura, kuhusu haki ya kupiga kura, anapeleka 'message' (ujumbe) gani kwa wafuasi wake? Uongozi ni mfano.
“Inakuwaje kiongozi ambaye ni mwanasheria, anajua haki, anajua demokrasia, anaikataa haki yake ya kupiga kura? Kwa hiyo, inaingia katika rekodi kuwa hatopiga kura katika nchi hii kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, lakini tutarajie kelele za kuhoji matokeo, wakati hata kura yake hana,” alisema hivyo Makalla Oktoba 22, mwaka huu.
Akijibu hoja hiyo, Lissu alisema: "Kutokujiandikisha kupiga kura hakumwondolei mtu yeyote haki ya kuzungumza chochote kuhusiana na utaratibu wa uchaguzi husika, kama ambavyo haimwondolei mtu yeyote haki ya kuzungumzia mambo yoyote yanayohusu umma katika nchi yetu.
"Uchaguzi wetu unazungumziwa si tu na watu wanaopiga kura kwenye uchaguzi huo, isipokuwa unazungumziwa pia na jumuiya ya kimataifa. Ndio maana huwa wanakuja watu kutoka nje ya nchi kuja kutazama uchaguzi huo kama ni huru na haki kiasi gani.
"Uchaguzi huo unazungumzwa na kwenye vyombo vya habari vya ndani na nje, na si kila mtu anayezungumzia uchaguzi wetu ni mtu mwenye haki ya kupiga kura au ya kuchaguliwa," alisema Lissu.
Mtaalamu huyo wa sheria alisema kuwa kabla ya kuondoka kwenda Ubelgiji Oktoba 2 mwaka huu, alikuwa akitoa elimu kwa viongozi wa chama chake kwenye Jimbo la Kibamba, hivyo katika uchaguzi ambao chama chake kinaweka nguvu, ni pamoja na huo wa serikali za mitaa.
“Ile siku niliyoondoka, kabla sijaenda uwanja wa ndege kusafiri, nilikuwa ninafanya mafunzo ya viongozi na watia nia wa kugombea uchaguzi huo katika Jimbo la Kibamba la mkoa wa Dar es Salaam.
"Hiyo inakuonesha ni jinsi gani ambavyo ninautilia maanani uchaguzi huo, na hayo mafunzo nimeyafanya si Kibamba tu, nimeyafanya kwa viongozi wa ngazi za kanda, makao makuu ya chama, nimeyafanya jimboni kwangu Singida Mashariki na nimeyafanya Singida Kaskazini.
“Kwa hiyo, mtu anayesema sitilii maanani kwa sababu tu nimeshindwa kujiandikisha kupiga kura kutokana na hayo niliyoeleza...” alisema Lissu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED