Mfumo wa elimu nchini wakosolewa

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 11:55 AM Nov 05 2024
   Mfumo wa elimu nchini wakosolewa
Picha:Mtandao
Mfumo wa elimu nchini wakosolewa

MBUNGE wa Kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha, amekosoa mfumo wa elimu kuwa ni tatizo kutokana na masomo kufundishwa "kijumla jumla" na kutokuwa na uhusiano wa moja kwa moja na kupunguza umaskini.

Akichangia mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/26, alisema njia mwafaka ya kuongeza tija katika uzalishaji iwe katika sekta ya kilimo au viwanda ni kuwekeza kwenye elimu bora inayosisitiza ufundi na ugunduzi.

“Ni bahati mbaya elimu yetu bado haikidhi kiwango hicho cha ubora na mara nyingi tunafundisha masomo ya jumla badala ya yanayosisitiza ujuzi, weledi na umahiri, tunatumia wastani wa Sh. bilioni 500 kila mwaka kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na fedha hizi mchango wake ni mdogo katika kukuza uchumi,” alisema.

“Tatizo letu ni nini, tunafundisha masomo ya jumla jumla ambayo hayana uhusiano wa moja kwa moja katika kupunguza umaskini, nilitarajia tungefundisha usimamizi wa mipango, usimamizi wa maendeleo, usimamizi wa rasilimali watu, usimamizi wa viwanda na usimamizi wa sekta ya afya na ndiyo ambayo yanahusiana na kupunguza umasikini.”

Vile vile, alisema alitarajia wafundishwe masomo ya ukalimani, ufundishaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni ili watafsirie wataalamu nchi za ughaibuni na kwa upande wa teknolojia alitarajia wafundishwe vijana masuala ya sayansi ya data na akili bandia.

Alisema Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kina shule nzima ya teknolojia ya habari na wakati huo huo Wizara ya Habari na Teknolojia ya Habari inajenga chuo cha umahiri cha teknolojia na Tehama na kudai kuwa ni matumizi mabaya ya fedha.

“Kwa maoni yangu, haya ni matumizi mabaya sana ya rasilimali za taifa, ingekuwa vizuri kama taifa tungegawa vyuo vikuu kulingana na weledi na ubobezi wa masomo, UDOM kingefundisha masuala ya sayansi, teknolojia na uvumbuzi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kingefundisha masomo ya Sayansi ya Jamii, Muhimbili kikaendelea kama kilivyo na SUA kikaendelea kama kilivyo,” alisema.

Alisema pamoja na Wizara ya Elimu kuwa na dhamira ya kufundisha masomo ya ufundi na amali katika shule zote za sekondari na kuwa na vyuo vya VETA Tanzania nzima, lakini uwezo haupo wa kutekeleza jambo hilo.

MATUMIZI MZIGO

Alisema baadhi ya matumizi ya serikali kwa maoni yake yanaibebesha serikali mzigo mkubwa badala ya kusaidia kuongeza tija.

“Mfano Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Maliasili, Wizara ya Maji wananunua mitambo inayofanana na wote wanafanya kazi ya kuchimba mabwawa na kutengeneza barabara.”

“Baada ya muda mfupi tu, vifaa vinaanza kutelekezwa porini kwa sababu ya gharama za mafuta na gharama za matengenezo zimekuwa kubwa sana badala ya vifaa hivyo kuwekwa sehemu moja na kila anayehitaji atakodi,” alisema. 

Alisema licha ya Wizara ya Kilimo kupatiwa wastani wa Sh. trilioni moja kila mwaka kwa ajili ya maendeleo ya kilimo, tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo bado iko chini sana.

Naye Mbunge wa Mahonda (CCM), Abdullah Ali Mwinyi, alisema elimu ya chuo kikuu haina umuhimu mkubwa kwenye ajira na kampuni zote kubwa kwa kuwa wanaangalia suala la ujuzi.

MIRADI KIMKAKATI

Mbunge wa Kuteuliwa, Prof. Shukrani Manya alitaka utashi uliotumika kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya Reli ya Kisasa (SGR) na Bwawa la Mwalimu Nyerere ufanyike kwenye miradi ya Liganga na Mradi wa Kusindika na Kuchakata Gesi (LNG).

Alisema mradi wa LNG ukikamilika au kuanza mapema ni kichocheo cha viwanda vya mbolea na kemikali na kuokoa fedha zinazotumika kuagiza mbolea nje ya nchi.

“Mradi wa Chuma wa Liganga umekuwa ukitajwa mwaka hadi mwaka kwenye mipango na bajeti ya serikali, tunajenga reli kwa kutumia chuma nyingi sana, kwa utashi ambao serikali imefanikisha kwa miradi mikubwa basi miradi hii mingine nayo ambayo imeendelea kuongelewa mwaka hadi mwaka, Prof. Mkumbo (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, huu mpango useme ni lini, tusiendelee kuwa tunahamisha, tunapanga, tuseme lini,” alisema.

Kuhusu kubana matumizi fedha za uendeshaji, Prof. Manya alisema kutokana na kuwa na umeme unaotosheleza mahitaji, anapendekeza Mamlaka za Maji zipewe tariff maalum ya umeme ili kupunguza wananchi wapate maji kwa gharama nafuu.

Naye Mbunge wa Ludewa (CCM), Joseph Kamonga, aliomba serikali iongeze kasi ya utekelezaji kwenye mradi wa Liganga na mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma.

Mbunge wa Ndanda (CCM), Cecil Mwambe, alisema mradi wa Liganga na Mchuchuma kwa sasa ni zaidi ya miaka 50 tangu akiwa mdogo unaongelewa na kwamba kwa sasa wanataka waone utekelezaji wa mradi huo ili uwe na tija.