Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi , amesema Serikali imedhamiria kuboresha mawasiliano hususani maeneo ya vijijini ili kuwaunganisha wananchi kwa lengo la kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kidijitali.
Mahundi ameyasema hayo mkoani Morogoro alipofanya ziara ya kikazi, kukagua minara iliyojengwa katika Kata ya Mikese wilaya ya Morogoro na Kata ya Lubungo wilaya ya Mvomero, ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 unatekelezwa na Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote (UCSAF) kwa usimamizi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP).
Awali, akitoa taarifa ya Utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji, Utafiti na Maendeleo wa UCSAF, Mhandisi Albert Richard amesema, minara hiyo imejengwa kwa teknolojia ya 2G, 3G, na 4G na kuongeza kuwa katika kata ya Lubungo Serikali imetoa ruzuku ya sh. milioni 360 ili kujenga minara miwili, mmoja umejengwa katika kijiji cha Lubungo na tayari umekamilika, na mnara mwingine unajengwa katika kijiji cha Vianzi, ambako utekelezaji unaendelea.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED