ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Isaack Amani amewataka wanandoa kuacha tabia ya kuangamizana kwa kuua kwa kukosa upendo.
Pia amewataka wanandoa kuacha tabia ya kuendekeza michepuko" kwa kuwa kufanya hivyo ni kukosa upendo.
Askofu Amani alikemea hayo jana usiku wakati wa misa ya mkesha wa Sikukuu ya Krimasi iliyofanyika katika Parokia ya Tokeo la Bwana iliyoko Burka, jijini hapa.
Aliwataka wanandoa kuacha visa na ugomvi unaosababisha baadhi yao kuangamizana kwa kutoa roho kwa namna tofauti.
Askofu Amani alisema mojawapo ya sababu za kuangamizana ni kukosa upendo ndani ya ndoa na kuwasababisha kuchepuka, kuamsha hasira na kuchukua hatua za kuuana.
Vilevile, aliwataka watoto kuacha tabia ya kuwahisi wazazi wao kuwa ni wachawi na badala yake kufuata kwa umakini amri za Mungu za kuwapenda wazazi na kuwaheshimu.
"Matokeo ya kukosa upendo, kuchepuka, kuuana, ubinafsi na uchawi ni ukatili wa hali ya juu ambao haujengi kabisa taifa lenye nguvu. Yesu amezaliwa kwa ajili yetu, ameleta upendo wa Mungu tuuishi ili kuleta amani na mapatano miongoni mwetu," alisema.
Vilevile Askofu Amani ameelekeza familia ziepuka kuepuka kuwa vichaka vya kuficha uhalifu na kuumizana ili kuishi maisha ya Yesu Kristo.
Alielekeza hayo jana asubuhi jijini Arusha wakati wa mahuburi ya maadhimisho ya Misa ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Theresia wa Mtoto wa Yesu.
"Familiya inatakiwa kuwa mahali salama pa kustahimili, kujifunza utu, kazi na kuheshimiana na kupeana msamaha, haya ndio mambo ya msingi kitika familia, si kichaka cha kuficha uhalifu na kuumizana," alisema.
Alisema ukatili wa majumbani kwenye familia umeenea kote nchini na dunian, utamaduni wa kufichiana siri kwenye ukoo kisa kutoaibisha na kuogopa kutumia sheria unasababisha kuficha uhalifu na ukatili katika familia.
Alishauri watu kujenga utamaduni wa kutumia vyombo vya sheria kutatua migogoro inayojitokea badala ya kumalizana kiukoo kwa lengo la kuficha uhalifu.
Askofu Amani alisema sikukuu ya Krismasi ni fursa kwa wafanyabiashara na huleta furaha, hivyo itumike vyema kuleta amani.
"Utasikia nyimbo zinaimbwa madukani, vyombo vya usafiri na wafanyabiashara wanapata fursa ya kuuza vitu mbalimbali, hivyo kila mtu anapata furaha. Tuitumie kuendeleza furaha na amani," alisema.
Pia aliwaasa waumini hao kukataa tamaa katika maisha yao, badala yake kila mmoja ahakikishe anaishi kwa haki katika ulimwengu wa sasa.
Alitumia mahubiri hayo kuwaasa vijana wanapojiandaa kwa maisha, wajipe muda wa kujifunza stadi za maisha na hasa kazi wanazohitaji.
"Unakuta kijana anaomba kazi, ukimwuliza 'kazi gani?" anajibu 'yoyote'. Nimwuliza kudeki unaweza 'siwezi', kupika 'siwezi'. Sasa unashindwa kumwelewa. Ninaomba watumie muda kujitafakari si kwenda haraka haraka.
"Hata kwa baadhi ya mabinti unakuta anataka kuingia katika ndoa lakini hajajiandaa kuwa katika ndoa, matokeo yake anaingia katika ndoa inavunjika siku mbili kwa sababu hajajiandaa wala hajajipa muda kujitafakari," alisema.
Askofu huyo pia alisema jamii inapita katika changamoto ya rushwa na Ukimwi ambao unasambaa kwa kasi aliyoita "ya ajabu".
Alisema kwa sasa rushwa imekuwa jambo la lazima, watu hunyimwa haki kwa kukataa kutoa chochote na inaweza kugharimu hata maisha ya mtu kwa kukataa kutoa rushwa.
Kwa upande wa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), Askofu Amani alisema yanazidi kusambaa katika jamii kwa sababu ya kujiachia kwa tamaa.
"Hii inasababishwa na marafiki wanaishi kama watu wa ndoa na wachumba wanaishi kama watu wa ndoa. Hii ni tamaa! Neno linatuasa usizifuate tamaa za mwili, bali jizuie na tamaa mbaya, ili tuishi kwa amani na furaha," alionya.
*Imeandaliwa na Daniel Sabuni na Cynthia Mwilolezi
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED