JKT Tanzania yalia refa amewamaliza

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 09:21 AM Dec 26 2024
Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Hamad Ally
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Hamad Ally

KOCHA Mkuu wa JKT Tanzania, Hamad Ally, amesema hajafurahishwa na matokeo waliyoyapata katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba iliyochezwa juzi na kuahidi kujipanga vyema kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi hiyo.

Simba ikiwa mwenyeji wa mechi hiyo ya kiporo ilipata ushindi wa bao 1-0, Jean Ahoua, akifunga kwa penalti dakika za lala salama.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ally alisema aliwaandaa vyema wachezaji wake isipokuwa bahati haikuwa upande wao na kuwataka mashabiki wasikatishwe tamaa.

"Malengo yalikuwa ni kumaliza mzunguko huu kwa ushindi, isipokuwa imekuwa tofauti, kilichobaki kwa sasa tunakwenda kujipanga kwa ajili ya mzunguko wa pili ili tumaliza katika nafasi za juu katika msimamo wa ligi," alisema Ally. 

Kocha huyo alisema licha ya kupoteza mchezo huo hajakata tamaa kwa sababu anakwenda kufanyia kazi mapungufu aliyoyabaini ili wafanye vizuri kwenye mzunguko wa pili ambao ndio unafunga hesabu za msimu. 

Naye Ofisa Habari wa JKT Tanzania, Masau Bwire, alisema hajaridhishwa na ushindi walioupata Wekundu wa Msimbazi kwa kuelekeza mwamuzi wa mchezo huo hakuwatendea haki. 

"Sijaridhishwa na maamuzi yaliyofanywa na mwamuzi wa mchezo huu mpaka kutufanya tupoteze mchezo wetu wa leo (juzi)," alisema Bwire.

Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi 37 na kuendelea kujiimarisha katika msimamo wa Ligi Kuu Bara huku JKT Tanzania yenye pointi 19 ikiwa katika nafasi ya nane baada ya kukamilisha michezo yake ya mzunguko wa kwanza.

Kagera Sugar yenye pointi 11 sawa na Tanzania Prisons na KenGold yenye pointi sita zinazubura mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo yenye timu 16.

Ligi Kuu Bara inatarajia kuendelea tena leo kwa Azam FC kuwakaribisha JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.