Bingwa Dk. Mngumi na darasa la unywaji sahihi maji yasikudhuru

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 08:35 AM Dec 26 2024
Dk. Jonathan Mngumi, Tabibu Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, na Figo, na anayeongoza kitengo cha magonjwa hayo, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
Picha: Mpigapicha Wetu
Dk. Jonathan Mngumi, Tabibu Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, na Figo, na anayeongoza kitengo cha magonjwa hayo, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)

JUZI Jumanne, gazeti hili lilikuwa na ufafanuzi namna ilivyo thamani ya maji, ikiendana na tahadhari ya ama kuzidisha kunywa au kupunguza mahitaji, huangukia madhara. Fuatilia...

Dk. Jonathan Mngumi, Tabibu Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Mbobezi wa Magonjwa ya Figo, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ana darasa zaidi kuhusu kiwango cha unywaji maji kuzingatia mazingira, aina ya kazi.

Huku akiendeleza anagalizo lake la juzi ‘kutopitiliza unywaji maji,’ anadadavua jinsi maji yanavyopunguza ukavu wa ngozi, kudumisha afya ya viungo kama magoti na viwiko, akihimzia ‘tii kiu yako kwanza, kabla ya kunywa maji.’

Bingwa huyo anayeongoza Kitengo cha Magonjwa ya Figo, katika maelezo yake kwa Nipashe wiki hii, anataja mbinu, faida na athari za kutokunywa maji pamoja na mfumo mzima wa figo na mkojo. 

“Faida za maji ya kunywa kwa binadamu, kwanza maji ni muhimu kwa uhai na afya ya mwili. Faida zake ni uwezo wa kutoa sumu mwilini, maji husaidia figo kuchuja taka na sumu kutoka kwenye damu na kuzitoa kupitia mkojo,” anasema bingwa huyo

Dk. Mngumi, anafafanua kuwa maji yanasaidia mzunguko wa damu, kudumisha ujazo wake na kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.  

Pia, maji yanasaidia kuboresha na kufanikisha mmeng'enyo wa chakula, ikizuia tatizo la kufunga choo na inadhibiti joto la mwili.

“Maji husaidia kupooza mwili kupitia jasho, hasa wakati wa joto kali au mazoezi, kulainisha viungo na kuimarisha ngozi. Hupunguza ukavu wa ngozi na kudumisha afya ya viungo kama magoti na viwiko,” anasema.  

KIASI KINACHOHITAJIKA

Bingwa huyo anasema, mtu mzima anayefanya kazi nzito juani au kutokwa jasho jingi, anashauriwa kunywa maji kati ya lita tatu hadi tano kwa siku, kulingana na kiwango cha jasho na unyevunyevu wa mazingira.  

Unywaji maji
Anasema, mbinu ya upimaji maji na namna ya kunywa ni angalau glasi moja hadi mbili za maji kila saa. Vilevile, kila baada ya saa moja ya kufanya kazi nzito, anatakiwa kunywa takribani mililita 500 (nusu lita) mpaka lita moja za maji.  

Dk. Mngumi anabainisha, iwapo kiu ni zaidi au mkojo una rangi tofauti, akitoa mbinu ya kuchunguza kuwa: “Ikiwa mtu anajisikia kiu sana au mkojo wake ni wa rangi ya njano iliyokolea, ni dalili ya ukosefu wa maji mwilini na anapaswa kuongeza unywaji wa maji. “ 

UNYWAJI USIO SAHIHI 

Dk. Mngumi anaeleza athari za unywaji duni wa maji, akisema unaweza kuathiri viungo kadhaa ambavyo ni muhimu.  

“Figo; ukosefu wa maji huongeza hatari ya mawe kwenye figo (kidney stones), maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) na kushindwa kufanya kazi ipasavyo.  

AI
“Ngozi; ukosefu wa maji hufanya ngozi kuwa kavu na kuharakisha kuzeeka,“anatamka na kuendelea:“Moyo; huongeza mzigo kwa moyo kwa sababu ya kupungua kwa ujazo wa damu, jambo linaloweza kusababisha shinikizo la damu.”  

Mtaalamu huyo anaendelea: “Ubongo; upungufu wa maji unaweza kusababisha maumivu ya kichwa, kutoelewa vizuri na uchovu.  

“Mmeng'enyo wa chakula; Unywaji duni husababisha kufunga choo na kuongeza asidi (tindikali) tumboni, jambo linaloweza kusababisha vidonda vya tumbo.”  

 WASTANI WA KUJISAIDIA 

Dk. Mngumi anataja idadi ya safari za kwenda haja ndogo kwa saa 12 hadi 24, kwa mtu kila siku akiainisha kwa lugha: “Kwa mtu mwenye afya njema, kujisaidia haja ndogo mara nne hadi saba kwa siku ni kawaida. Sawa na kila baada ya saa tatu hadi nne.  

“Kwa saa 12 kujisaidia mara mbili hadi nne, kwa saa 24, kujisaidia mara nne hadi saba7, kulingana na kiwango cha unywaji maji na shughuli za mwili ni kawaida.  

“Ishara za tatizo ni ikiwa mkojo ni wa rangi ya njano iliyokolea au kujisaidia ni mara chache sana (chini ya mara nne kwa siku), huenda mtu anakunywa maji ‘machache’ (kidogo).” 

 UNYWAJI DUNI

Bingwa huyo anasema kuna athari ya kutokunywa maji, akiutolea maelezo kuwa “unywaji duni wa maji, huathiri mfumo wa mkojo kuanzia kwenye figo hadi kibofu, pamoja na figo.”,  

Anataja eneo lingine la tatizo ni kwenye hatari ya kutengeneza mawe kwenye figo na husababisha kushindwa kuchuja sumu ipasavyo, jambo linaloweza kusababisha matatizo ya figo sugu (CKD).  

“Mirija ya mkojo (Ureter) huathiriwa, ukosefu wa maji huongeza uwezekano wa maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), hasa kwa wanawake,” anaeleza.

KIWANGO MAJI, KIBOFU

Dk. Mngumi anasema, kutokunywa maji kwa usahihi, kunasababisha maambukizi kutokana na mkojo kukaa muda mrefu kibofuni bila kutolewa.  

 Pia, anataja kupunguza uwezo wa kibofu kufanya kazi inavyotakiwa, jambo linalosababisha hisia ya haja ndogo mara kwa mara.  

“Kunywa maji ya kutosha kila siku ni muhimu kwa afya ya mfumo wa mkojo na mwili kwa ujumla,” anasema.

Kuhusu unywaji maji kwa kiwango kilichopitiliza (overhydration au water intoxication), Dk. Mngumi anasema, hutokea mtu anapokunywa kiasi kikubwa cha maji kwa muda mfupi, mwili hauwezi kuyatoa au kuyasawazisha kwa njia ya mkojo.  

Hapo anataja kiwango sahihi kwa watu wazima ni kunywa zaidi ya lita tano kwa siku au zaidi ya lita moja hadi kufika lita na nusu kwa saa kunaweza kuwa hatari kiafya.  

“Athari kubwa hutokea wakati figo zinashindwa kuchuja maji zaidi ya kiwango 0.8 ya lita (milimita 80) hadi lita moja kwa saa,” anatamka na kuughanisdja na ufafanuzi wa ishara za kunywa maji kupitiliza kiwango.

Anataja ishara za unywaji maji kupita kiasi ni; mkojo kupita kiasi na hutoka kila mara, ukiwa mweupe sana.  

Tatu; anataja mtu anavimba mwili wake, mikono, miguu au usoni; huku la nne, mtaalamu huyo anasema  anakuwa na hali ya kizunguzungu au maumivu ya kichwa, kutokana na kushuka viwango vya madini sodiamu kwenye damu.  

La tano, Dk. Mngumi analitaja kuwa, mtu anahisi uchovu wa mwili kwa kuwa mwili unajaa maji kupita kiasi na huathiri utendaji wa seli.  

Jambo la sita linaloathiri kunywa maji zaidi ni kuhisi kichefuchefu na kutapika. 

Saba, ni mtu kuwa na mawazo ya kuchanganyikiwa, baada ya kupungua kwa sodiamu kwenye damu (hyponatremia) huathiri kazi za ubongo.  

KUNYWA KUPITA KIASI 

Miongoni mwa madhara ya kunywa maji zaidi, bingwa huyo anasema ni maradhi anayoyataja kswa jina ‘Hyponatremia’ (kiwango kidogo cha sodaimu).

Kuwapo maji mengi, kunapunguza kiwango cha sodiamu kwenye damu, hali inayoweza kusababisha matatizo ya neva na misuli.  

Akisema matokeomabaya zaidi ni mtu kupata kifafa au kupoteza fahamu na inaweza kumletea hali ya kuvimba ubongo (Cerebral Edema). Kushuka kwa sodiamu, kunatajwa kitaalamu kunasababisha maji kuingia ndani ya seli za ubongo na hivyo ubongo huvimba. 

AI
“Hali hii inaweza kuwa hatari kwa maisha.  Kazi za figo kushuka. Figo hufanya kazi kupita kiasi kujaribu kutoa maji mengi, jambo linaloweza kusababisha uchovu wa figo.  

“Kushindwa kupumua, maji kupita kiasi yanaweza kujikusanya kwenye mapafu, hali inayosababisha ugumu wa kupumua.  

“Madhara kwa moyo. Ujazo wa damu unaongezeka, hivyo moyo hulazimika kufanya kazi zaidi, jambo linaloweza kuleta matatizo ya moyo,” anatamka  

KUEPUKA UNYWAJI ULIOPITILIZA

Dk. Mngumi anasema ziko njia za kufuata kuepuka kunywa maji kupitiliza, ikianzia na kusikiliza mahitaji ya mwili.

“Kunywa maji taratibu: Usinywe maji mengi kwa wakati mmoja, badala yake kunywa mara kwa mara kwa kiasi kidogo.  

“Kufuata hisia za kiu: Kunywa maji pale unapohisi kiu badala ya kulazimisha kunywa.  

“Kuangalia dalili za ‘overhydration’: Ikiwa unahisi dalili kama kizunguzungu, maumivu ya kichwa au uvimbe, punguza unywaji maji na tafuta ushauri wa daktari.  

“Unywaji maji kupita kiasi ni hatari kwa mwili na unapaswa kusimamiwa kwa uangalifu, ili kuepuka madhara.

“Vilevile, kuna watu kutokana na changamoto za magonjwa mfano ugonjwa wa figo, watashauriwa kupunguza na kunywa maji yasiyozidi lita moja, kwa saa 24,” anasema.

Pia, anasema kuna ushauri wa kunyw maji wakati wa mchana zaidi, kwani kuna upotevu na haja ya kuyarudishia mwilini na sio kukesha kunywa maji usiku.

“Unywaji wa maji ‘0.5 lita (nusu lita) hadi lita tatu' kwa mtu wa kawaida, inatosha, labda awe na sababu za kitaalamu au aina ya kazi anayo ifanya ilete uhitaji wa maji zaidi,” anamaliza.