MAHUBIRI ya mkesha wa Krismasi yametawaliwa na nasaha juu ya kulinda amani na upendo huku viongozi wa dini wakiwataka watanzania kudhibiti na kukemea vitendo vya rushwa, utekaji na uvunjifu wa amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Akihutubia waamini wakatoliki wakati wa mkesha jana katika Kanisa la Bikira Maria Malikia wa Amani, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Flaviani Kasala alisema sikukuu ya Krisimasi inatakiwa kutumika na watanzania wote kujirudi kwa kukataa matendo maovu yanayoharibu taswira ya taifa.
Alisema matendo hayo ni pamoja na rushwa kwa kuwa watanzania wanaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, hivyo wakiendekeza rushwa, hakutapatikana viongozi walio na nia ya dhati ya kulitumikia taifa.
Askofu Kasala alitolea mfano Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka huu nchini, akisisitiza kuwa ulionekana kuwa na dosari nyingi, ikiwamo watu kushawishiwa kwa rushwa. Alisema dosari hizo hazipaswi kujitokeza katika Uchaguzi Mkuu.
"Tusikubali kugawanywa wala kutenganishwa na wanasiasa pale tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 badala yake tudumishe amani, upendo na mshikamano," alisema Askofu Kasala.
Kuhusu matukio ya utekaji, Askofu Kasala alisema ni ishara mbaya kwa taifa linaloaminika kuwa kisiwa cha amani, hivyo kuhimiza vitendo hivyo vidhibitiwe na uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu.
Aliwataka waamini wa kanisa hilo kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kudumisha amani, upendo, mshikamano na kuheshimiana wakati wote kama maandiko matakatifu yanavyoelekeza.
Alisema kuwa kupitia sikukuu ya Krisimas ya kumbukizi ya kuzaliwa Yesu Kristo, ni vyema kila mmoja akajiuliza na kutafakari na kwenda kutenda mema yanayompendeza Mungu.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi, katika salamu zake za Krismasi, alisema sherehe hizo si tu za wakatoliki au madhehebu mengine yanayosherehekea, bali zinamhusu kila mmoja kutokana na imani ya ukombozi iliyozaliwa katika Kristo kwa watu wote.
"Kristo ni nuru inayotuangazia sisi ili na sisi tuiangaze kwa wengine na nuru hiyo inaangazwa kwa wote pamoja na madhehebu mengine kwani yeye hakuwapo kwa wale wanaompenda bali wote kwani alimwaga damu yake ili wote tusamehewe dhambi," alisema Askofu Niwemugizi.
Alisema kuwa katika kujitoa ni lazima kujitoa kwa watu wote, akitolea mfano katika mahubiri kuwa kutoa kwa rafiki tu hakuna ulichokifanya bali kwa wote wenye uhitaji.
Mkoani Mwanza, Paroko Msaidizi wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Karoli Luhanga, Nyegezi Jimbo Kuu la Mwanza, Switbert Massao alisema anapozaliwa Mfalme wa Amani, iko haja kila mtanzania kujiuliza kama kuna amani na kuchukua hatua.
Padri Massao alisema kama taifa watu wamejawa na mawazo mbalimbali ambayo yanadhihirisha kupungua kwa hali ya amani kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
"Mtu anatoka nyumbani anabaki anawaza 'nguo zangu nimeziacha kwenye kamba, sijuhi nitazikuta', mwingine anatembea anawaza 'sijui mume/mke kwa sasa yuko wapi na anafanya nini'.
"Huo ni wivu na kutokuaminiana, yote hayo yakiwamo na mambo ya wizi, utekaji na vita yanamfanya mtu kukosa amani kutokana na ulimwengu wa sasa kuwa wa kutisha kwa kila mtu," alisema Padri Massao.
Alisema iko haja kuhakikisha kunakuwa na amani nchini na kwenye familia, akisisitiza kuwa nyumba yenye amani inapata wageni, lakini ili yenye vurugu hakuna mgeni atakayetamani kuisogelea.
"Tuhakikishe tunachukua baraka za kuzaliwa kwa Kristo kwa kuishi na kudumisha amani na upendo kwani Kristo ni wa amani, upendo na baraka," alisema Padri Massao.
Paroko wa Kanisa Katoliki Ngokolo, mjini Shinyanga, Adolf Kamandagu, akihutubia waamini katika Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma Ngokolo, aliwasisitiza watanzania kuendelea kudumisha amani ya nchi.
Alisema chimbuko la amani ni Yesu Kristo ambaye alizaliwa kwa ajili ya kukomboa ulimwengu ambao ulikuwa umeanguka dhambini, hivyo ni vyema wanadamu wote wakaenzi amani hiyo.
"Yesu amezaliwa awe mbaraka kwetu, na ndiye mfalme wa amani. Tusheherekee sikukuu ya Krismasi kwa amani, tuendelee kuomba baraka katika nchi yetu, na amani iendelee kudumu," alisema Paroko Makandagu.
Pia aliwataka watanzania warudishe uhusiano wao na Mungu wao, na kuacha kutenda mambo maovu, bali wapendane, wasiendekeze chuki, viburi na wasitawaliwe na tamaa za kidunia.
Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Yesu Kristo Mchungaji Mwema iliyoko Kata ya Buhanda, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Achiles Charukula, alisema si kila ugumu wa maisha unasababishwa na laana kutoka kwa Mungu au wazazi, bali ni mpango wa Mungu katika kumwinua mja wake.
Padri Charukula alisema katika kutilitambua hilo ni vyema waamini wa kanisa hilo pamoja na watanzania wote kumrejea Mungu wakati wote na si kuhangaishwa na matatizo pamoja na mahitaji ya jambo fulani.
"Ukiwa mnyenyekevu na mstahimilivu katika matatizo ni kipimo cha Mungu juu ya uvumilivu wako na wala si laana wala nini, hivyo yeye ndiye ataruhusu upate kile kilicho chema kwa ajili yako," alisema Padri Charukula.
Alisema kipindi kigumu katika maisha kiwe chachu ya kumtafuta Mungu na kujua kusudi lake ndani ya mtu badala ya kulalamika na kwamba katika kipindi hicho utukufu wa Mungu huonekana.
Padri huyo pia alitoa wito kwa wanaume wenye familia kutozikimbia pale maisha yanapobadilika na kuwa magumu badala yake uwe ni wakati ambao watashikamana kama ambavyo Yusufu alishikamana na mkewe Mariam katika kipindi kigumu cha kuzaliwa kwa Yesu Krito mkombozi.
Kiongozi huyo wa kiroho pia aliwataka wanawake wote walio na ujauzito, wautunze kwa kula chakula bora na kufanya mazoezi kwa ajili ya kumtunza mtoto aliye tumboni kwa kuwa hakuna mwanamke anayejua amebeba mtoto mwenye hatima gani.
MAKAMU WA RAIS
MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango na mkewe, Mama Mbonimpaye Mpango jana waliungana na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska, Kiwanja cha Ndege, mkoani Dodoma katika ibada ya sikukuu ya Krismasi.
Akitoa salamu za sikukuu ya Krismasi kupitia kwa waumini hao, Makamu wa Rais aliungana na Rais Samia Suluhu Hassan kuwatakia wakristo na wananchi wote heri ya sikukuu ya Krismasi.
Aliwataka watanzania kusheherekea sikukuu kwa amani na utulivu pamoja na kujitoa kusaidia wale wasio na uwezo.
Makamu wa Rais pia alitoa wito kwa watanzania kutumia sikukuu ya Krismasi kutafakari juu ya malezi ya watoto majumbani kwa kuwaepusha na vitendo vya ukatili wanavyopitia.
Alisema ni vyema kutafakari nafasi ya watoto katika taifa kwa kuwapelekea tumaini, amani, upendo na furaha.
Makamu wa Rais pia alitoa rai kwa vyombo vya usalama kusimamia vyema sheria za usalama barabarani ili watanzania washerehekee sikukuu kwa amani.
*Imeandaliwa na Alphonce Kabilondo (GEITA), Daniel Limbe (CHATO), Marco Maduhu (SHINYANGA), Adela Madyane (KIGOMA), Vitus Audax (MWANZA)
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED