MATUMIZI ya njia za uzazi wa mpango, unatajwa si jukumu la mwanamke pekee, bali jambo linalobeba usawa wa kijinsia.
Hapo wanaume nao wana njia za uzazi wa mpango wanazoweza kuzitumia, katika kuwapuguzia wanawake majukumu na adha ya kupata matatizo ya kiafya.
Wajibu wa wanaume ni kuwasaidia wanawake kutumia njia za uzazi wa mpango, ili kutokomeza kupata mimba zisizotarajiwa.
Ni hatua muhimu inayowasaidia wanawake kupata afya bora ya uzazi na kuleta manufaa kwa jamii kiujumla, katika sura pana kitaifa.
Mara zote imekuwa kawaida kwa wanaume, kuwaachia wanawake zao mambo yote yanayohusiana na uzazi.
Ni mtazamo unaotawala kwamba, si jambo la wanawake pekee, wala si wanaume, lakini uhalisia ni kwa wanaume wanapaswa kushiriki vema mambo ya uzazi wa mpango.
Wataalamu afya na mamlaka zenye dhamana kwa kuliona hilo, wameendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya uzazi wa mpango.
Pia, nafasi ya wanaume katika kutumia uzazi wa mpango, kuwezesha uzazi salama kwa mama pamoja na mtoto.
Hata hivyo, mbali na elimu hiyo, pia kunatajwa hitaji kufunga uzazi, pindi wanapofikia ukomo wa kuhitaji watoto, ili kuepuka mimba zisizo tarajiwa kwa wakati usio sahihi.
WATAALAMU HUDUMA
Kwa mujibu wa mtaalamu kutoka Manispaa ya Mkoa wa Kahama, Dk. Noel Malaki, anasema idadi ya wanaume wanaohudumia katika masuala ya uzazi wa mpango ni ndogo, ikilinganishwa na idadi ya wanawake katika mji huo.
Akifafanua, anasema kutokana na uhaba wa elimu kuhusu kufunga uzazi kwa wanaume haijatolewa ipasavyo, hivyo ni sababu inayochangia kutotumiwa na wadau wa kutosha.
Vilevile, Dk Malaki anataja matumizi ya uzazi wa mpango kuwa duni nako kunachangia kutoaminika kwake, kuwa njia sahihi, baadhi wakihofia uwezekano wa walakini katika tendo la ndoa kama awali.
Anataja mtazamo kwamba, baadhi ya njia za uzazi wa mpango ambazo mwanaume anaamini ni pamoja na matumizi ya kondomu, pia kutoa mbegu za kiume nje wakati wa tendo hilo, mwanamke akiwa kwenye siku za hatari kushika mimba.
Vilevile Dk. Malaki anataja kuwapo hali ya kufanyika upasuaji mdogo kwa lengo la kufunga mrija inayosafirisha mbegu za kiume; kitaalamu inaitwa (vasectomia).
Ni utaratibu wa upasuaji wa kufunga kizazi kwa mwanaume, walau miezi mitatu. Pia, viwango vya kutofaulu katika hatua hiyo, vinatajwa ni takribani moja kati ya 2000. Hiyo kwa ujumla, inaorodheshwa ni njia ya kudumu ya kupanga uzazi kwa sababu, inamfanya mtu asiweze kuzaa tena.
UTATA UZAZI KIUME
Dk Malaki, anasema ingawa kuna njia za kurejesha uzazi wa kiume, kuna mbinu ya kuchukua mapema mbegu ya kutunga baadaye mimba nje ya mwili (invitrofertization).
Hilo linashauriwa kwa vijana wasio na watoto, kwa sababu uwezekano wa kughairi, baadaye ni mkubwa zaidi.
Mtoa Huduma Ngazi ya Jamii, Clement Masonga, anasema huduma hiyo imekuwa ngumu kwa wanaume wengi, wanaokosa taarifa sahihi za ufungaji kizazi kwa wanaume, ndiyo sababu inayowafanya kushindwa kuitumia.
Anashauri nafasi ya wanaume kusaidia fedha za usafiri kwenda kulipia njia za uzazi wa mpango, ikiwamo mahudhurio ya kliniki, matumizi ya kondomu na nyenzo nyinginezo.
Mtaalamu huyo anasema, pamoja na wanaume wengi kuogopa kutumia njia hiyo, lakini uhalisia ndio njia rahisi na salama.
MNUFAIKA WA HUDUMA
Mnufaika wa huduma ya kufunga uzazi kwa wanaume na mkazi wa Kahama (jina tunalo), anaeleza alivyoitumia njia hiyo, baada ya kupatiwa elimu sahihi akinena akagundua haina madhara ya kushiriki tendo la ndoa na mkewe.
“Nilikubali kufunga kizazi kutokana na faida ambazo hapo awali sikuzifahamu. Pia, nilihofia kuwa nitashindwa kushiriki tendo la ndoa na mke wangu.
“Sasa nimeamini ni jambo la kawaida, pia linasaidia kutokomeza mimba zisizotarajiwa, hivyo nawashauri wanaume wenzangu kufunga uzazi,” anasema Samwel.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED