Fadlu awaita nyota Simba ni mashujaa, Kibu hauzwi ng'o

By Faustine Feliciane ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:18 AM Dec 26 2024
Kocha Mkuu Fadlu Davids
Picha: Simba SC
Kocha Mkuu Fadlu Davids

KOCHA Mkuu wa Simba, amewasifia wachezaji wake akisema wana tabia za kishujaa kwa sababu hawakati tamaa na wamejijengea tabia ya kucheza kwa kupambana mpaka filimbi ya mwisho, ameweka wazi kwa sasa, nyota wake, Kibu Denis, hauzwi.

Taarifa zilizopatikana jijini, Dar es Salaam jana zinasema Kibu, ambaye yuko Marekani kwa ruhusa maalumu anawindwa na Amazulu ya Afrika Kusini.

"Tayari klabu hiyo imeshafanya mazungumzo ya awali na Simba, lakini Fadlu ameweka wazi anamhitaji mchezaji huyo, yuko katika mipango yake," chanzo hicho kilisema.

Akizungumza baada ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania kumalizika juzi, Fadlu, alisema wachezaji wake wamekuwa na tabia ya kujituma na kucheza kwa malengo ya kusaka ushindi mpaka pale watakaposikia filimbi ya kumaliza mechi imelia huku akiwataka wanachama na mashabiki kuwa na moyo kama wao.

Kocha huyo alisema wachezaji wake wamekuwa na moyo wa kishujaa, kwa kuendelea kufanya mashambulizi makali licha ya ugumu wanaopata kutoka kwa wapinzani kwa lengo la kusaka ushindi hadi dakika za mwisho.

"Wachezaji wangu wameonesha fikra za kutokata tamaa, wanacheza kama mashujaa, wanapambana na kutokata tamaa hata kama dakika zinaelekea kumalizika, hata mashabiki wetu sasa wanapaswa kuwa na utamaduni kama wa wachezaji wao, kutokata tamaa hadi mwisho, hiki ndicho ninachotengeneza kwenye timu, angalia mechi kama tatu tunazimaliza kwa kupata ushindi mwishoni, dhidi ya Mashujaa, CS Sfaxien na leo (juzi)," alisema Fadlu.

Kuhusu mechi hiyo ya juzi ambayo walipata bao la jioni, Fadlu, raia wa Afrika Kusini aliisifu safu ya ulinzi ya JKT Tanzania ilikuwa ngumu kupitika, na Maafande hao walicheza zaidi nyuma na kushambulia kwa kushtukiza, hivyo kuwapa wakati mgumu.

Beki wa kati ya Simba, Abdulrazack Hamza, alieleza wazi walichokikuta uwanjani ni tofauti na kile walichotarajia.

Alisema ushindi huo umesaidia kuongeza pointi tatu na pia ugumu waliopata umewakumbusha timu sasa hivi zimejipanga sana hivyo wawe waangalifu.

Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi 37 na kuendelea kujiimarisha kileleni huku JKT Tanzania ikiwa nafasi ya nane na pointi zake 19 kibindoni.