Vita vya ‘unga’ Umoja Mataifa, AU hadi Samia afikia wa mfano kuigwa

By Tuntule Swebe , Nipashe
Published at 08:10 AM Dec 26 2024
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, akiwa na dawa za kulevya zilizoshikwa mkoani humo, Machi mwaka 2022.
Picha: Mtandao
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, akiwa na dawa za kulevya zilizoshikwa mkoani humo, Machi mwaka 2022.

NAMNA ya kuendesha maisha katika uhalisi wa kawaida, ina hatua inayopanda hadi mamlaka ya nchi, serikali na mkuu wake, vyote vikimrahisishia maisha mkazi, pia viumbe vingine kadri inavyowezekana.

Upande wa pili, kuna tafsiri inayomgusa moja kwa moja raia wa kawaida katika mwenendo wake wa kila siku. Hapo kuna dhana inayoitwa ‘watu kwenda na wakati’ wakijifunza matumizi ya vitu mbalimbali kama kompyuta zinazowarahisishia kazi.

Vilevile katika mageuzi hayo, kuna watu wanaofanya visivyostahili, wakiamini ‘ni mitindo ya kisasa.’ Hapo nako ndiko kuna hadithi kama matumizi ya pombe kupindukia, hali kadhalika dawa za kulevya, hatari kubwa kiafya.

Majumuisho ya misukumo ya fikra hizo, mtu anapotumia dawa za kulevya kwa falsafa ya ‘kwenda na wakati’, vyanzo vikuu vinavyomshawishi vikiwa vyombo vya mawasiliano; simu, televisheni, radio, simu na kompyuta inaibua mfumo mpya wa maisha.

DAWA KULEVYA IKOJE?

Dawa za kulevya ni kemikali, ziingiapo mwilini, huathiri ubongo wa mtumiaji na kumsababishia kuwa na matendo, hisia, fikra na mwonekano tofauti na matarajio ya jamii.

Kemikali hizo hutokana na mimea na madini ambayo ni malighafi muhimu kwa mahitaji mengine ya mwanadamu. Hizo zinapoingia mwilini kwa njia kuu tatu: Kunywa; kuzila dawa zisizoruhusiwa kama bhangi na mirungi, cocaine, heroin na mandrax; pia zinazoruhusiwa kwa tiba hospitali.

Umoja wa Mataifa unataja, zaidi ya watu milioni 296 walitumia dawa za kulevya mwaka 2021, ikiwa ni ongezeko la asilimia 23 kulinganisha na miaka 10 iliyotangulia, zikinukuu Ripoti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu - UNODC.

Takwimu mpya zikaweka makadirio ya kimataifa ya watu wanaojidunga dawa za kulevya kwa mwaka 2021 kwamba ni milioni 13.2; asilimia 18 juu kuliko ilivyokadiriwa awali. 
 
Ripoti hiyo inaeleza zaidi kwamba, idadi ya wanaougua shida za matumizi ya dawa za kulevya imepanda, kufika watu milioni 39.5, sawa na ongezeko la asilimia 45 katika kipindi cha miaka 10. 
 
UNODC inaangaza jinsi ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi, unavyosukumwa na changamoto za dawa za kulevya; uharibifu wa mazingira na ukiukwaji wa haki za binadamu, ukichangia pia, kuongezeka dawa za kulevya zinazotengenezwa viwandani. 

SURA YA TIBA

Mahitaji ya kutibu magonjwa yanayohusiana na dawa za kulevya yanaelezwa na Umoja Mataifa hayajafikiwa, wastani ukiwa mtu mmoja kati ya watano, wanaougua matatizo hayo (mwaka 2021) huku tofauti zinaongezeka katika upatikanaji tiba maeneo yote duniani.

Hapo kundi la vijana linatajwa kuwa hatarini zaidi kutumia dawa za kulevya, pia huathiriwa na magonjwa yanayohusu matumizi ya dawa hizo duniani. Barani Afrika kunatajwa kwamba, asilimia 70 ya wanaopata matibabu ya dawa za kulevya, wako chini ya umri wa miaka 35 au kwa lugha rahisi ni vijana. 

Ripoti inashauri afya ya umma, kinga na ufikiaji huduma za tiba, zipewe kipaumbele duniani, vinginevyo changamoto za dawa za kulevya zitaumiza wengi.

Kuna msisitizo unaotaja hatua za utekelezaji sheria, kuendana na mbinu za kudhibiti biashara ya uhalifu wa kisasa wa dawa za kulevya za bei nafuu zinazotengenezwa viwandani, ambazo ni rahisi kuletwa sokoni. 
  
Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC, Ghada Waly anafafanua: “Tunashuhudia kuendelea kuongezeka kwa idadi ya watu wanaokabiliwa na matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya duniani kote, huku matibabu yakishindwa kuwafikia wote wanaohitaji. 

“Tunahitaji kuongeza hatua dhidi ya makundi ya biashara ya dawa za kulevya yanayotumia mizozo na migogoro ya kimataifa, kupanua kilimo na uzalishaji haramu wa dawa za kulevya, hasa ya dawa za viwandani, kuchochea masoko haramu.”
 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, anatumia fursa hiyo kuisihi jamii kutowatenga waathirika wa dawa za kulevya, akiitaka jumuiya ya kimataifa kuendelea kukomesha matumizi mabaya na ulanguzi wa dawa za kulevya. 
 
SAMIA ANASIFIWA

Ndani ya hoja hiyo na harakati zake, kwa mustakabali wa Tanzania, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, anazitaka wizara zinazohusika na maendeleo ya jamii, pia asasi za kiraia.

Vilevile kuna suala la wazazi na walezi kuwekeza nguvu, kulinda jamii zao na kuendelea kudhibiti uingizaji, uzalishaji, usafirishaji na utumiaji dawa za kulevya.

Ni tamko lake Rais Dk. Samia katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Juni mwaka jana, katika kilele cha Maadhimisho Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani iliyobeba kaulimbiu ‘Zingatia Utu, Imarisha Huduma za Kinga na Tiba.”

Akasisitiza: “Kinga ni bora kuliko tiba, hivyo natoa wito kwa mamlaka husika, taasisi za serikali na asasi za kiraia kuongeza jitihada kwenye kutoa elimu kwa jamii hasa vijana wajiepushe na matumizi ya dawa za kulevya, lakini sisi serikali tumejipanga vyema kukabiliana na janga hili.” 

Rais Dk. Samia, pia akaipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), kufanya kazi nzuri ya kudhibiti uingizaji dawa hizo kitaifa.

Katika tukio hilo, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), iliwaelimisha wananchi waliotembelea kuhusu shughuli wanazozifanya, wakiwapima wahitaji na kutambua aina ya dawa hizo kutoka kwa waathirika kama heroin, bhangi na mirungi. Pia, wakawatambua watumiaji wapya.

Wakati kuna ufafanuzi huo wa mwaka jana wa mkuu wa nchi, mwezi huu Tanzania chini ya uongozi wake tena umemwagiwa sifa ya mafanikio kimataifa kupambana kukabili dawa za kulevya.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga, ametoa kauli hiyo jijini Arusha akifungua Mkutano wa Siku Nne wa jukwaa  lililo chini ya Umoja wa Afrika (AU), Tanzania ikitajwa kuwekeza zaidi kwenye kinga.

Anafafanua, maeneo yanakojengwa vituo vya kutoa huduma za afya kwa waraibu wa dawa hizo ni katika hospitali za kanda na rufani, makundi yakielimishwa, ikiwamo vilabu vya vijana shuleni.

Jukwaa hilo lina mikakati kupunguza uhitaji na usambazaji dawa za kulevya kwa nchi wanachama wa AU, Naibu Waziri anautaja ni mkutano unaotoa fursa ya kubadilishana uzoefu wa masuala ya afya, katika vita hivyo kukabili shida ya dawa za kulevya.

Naibu Waziri anataja mafanikio yametokana na kazi inayofanywa na Rais Dk. Samia, kuwekeza kwenye Sekta ya Afya, hususan ujenzi wa Vituo vya Tiba Saidizi kwa waathirika wa dawa za kulevya (MAT CLINICS) vinavyosimamiwa na serikali.

“Tumepiga hatua zaidi katika udhibiti wa dawa hizi nchini na wenzetu Nchi za Umoja wa Afrika, kuungana kwa pamoja katika kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya, kudhibiti mbinu wanazotumia wauzaji na watumiaji wa dawa hizo na uimarishwaji wa maeneo ya mipakani, kuzuia uingizwaji dawa hizo nchini kwetu,"anasema.

Anasema hatua zaidi zinaendelezwa na serikali kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya mitaani, sambamba na hatua za kisheria zinazochukuliwa.

“Jitihada za kudhibiti dawa hizi haziwezi kufanikiwa bila kushirikiana na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika ambazo ni nchi zote za Bara la Afrika zikiwamo Namibia, Botswana, Zambia, Nigeria, Kenya na Sierra Leone. 

“Kwa Tanzania kwa sasa tumeanzisha kituo cha utoaji huduma (Call Centre), ambako mwananchi ana uwezo wa kupiga simu kutoa taarifa za uwapo wa dawa za kulevya au viashiria, ili uchunguzi ufanyike na wahusike wachukuliwe hatua,” anasema Nderiananga

Katibu Mkuu Msaidizi, Mipango, Sera za Kimataifa anayeshughulikia Ofisi ya Afrika na Mashariki ya Kati katika Masuala ya Kimataifa ya Utekelezaji wa Sheria, (INL) Maggie Nadri anasema vifo vinavyotokana na matumizi ya dawa za kulevya yaliyopitiliza vimepungua kwa asilimia 12 katika nchi za AU.

“Ni wakati sasa wa kuongeza nguvu eneo la utoaji elimu kwa vijana shuleni, vyuoni ili kupunguza matumizi ya dawa hizi kwa kuwajengea uwezo wataalam wa afya na mamlaka za ulinzi kubadilishana mbinu za kudhibiti matumizi ya dawa hizo katika maeneo  ya  mipakani, majini, ardhini na  kwingineko ili kuwezesha wananchi wengi kutojiingiza katika dawa za kulevya,” anahitimisha Maggie.