KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, amewataka wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kuwa na subira.
Amesema watakaokatwa licha ya kushinda kura za maoni, wasiseme neno, badala yake wawe na uvumilivu kwa kuwa muda wao utafika, huku akiwatakia heri waliohamia vyama vingine, akidai kuwa ni suala la muda tu.
Mwenezi huyo pia amesema uchaguzi wa awamu hii hauna kupita bila kupingwa, hivyo wagombea na wanachama wa chama hicho wasibweteke, akisisitiza wako imara na hawatalala.
Makalla aliyasema hayo jana mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano wa chama wilayani Kinondoni, akisisitiza watahakikisha hata pale watakapokuwa peke yao, watafanya kampeni na kuhakikisha wagombea wao wanapata kura za "ndio".
"Anayesubiri kumwangusha mgombea wa CCM kwa kura za "hapana" ni sawa na mtu anayesubiri ndege bandarini badala ya ‘Airport’ (uwanja wa ndege). Wana CCM nchini kote tuchangamke, hakuna neno ‘mama’ tukamilishe hiyo kazi, mahali patakapothibitika tupo sisi tutafanya kampeni ya kutosha, wagombea wetu wote wapite kwa kishindo.
"Niwaombe tuendelee kufuatilia viongozi wetu wa matawi, kata, wilaya na mkoa, michakato inayoendelea sasa ya kupeleka wagombea katika maeneo hayo, itakapofika Novemba 21, mwaka huu tuanze kampeni za kistaarabu za kunadi mafanikio tuliyonayo na utekelezaji ilani ya uchaguzi. Kazi zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ni mtaji tosha wa kuipa CCM ushindi," alisema Makalla.
Aliongeza kuwa walifanya hamasa kubwa ya uandikishaji iliyofanikisha zaidi ya watu milioni tatu kuandikishwa ndani ya mkoa wa Dar es Salaam pekee, akieleza kuwa hamasa hiyo itakayotumika kufanya kampeni muda utakapofika, ifanywe kuwasisitiza wananchi kutoishia kwenye kijiandikisha badala yake wajitokeze pia kupiga kura.
Makalla alieleza kuwa chama hicho kinaamini kwamba Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni muhimu, hivyo wamejiwekea utaratimu maalumu ambao ulifanikisha kupata zaidi ya viongozi 500 watakaogombea katika maeneo mbalimbali kote nchini, akiwasisitiza kuonesha taswira nzuri kwa kuwa wameaminiwa.
Aliwapongeza baadhi ya wagombea ambao majina yao yalikatwa na wanaendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za chama hicho, akijitolea mfano yeye mwenyewe kwamba kuna kipindi aligombea na kushinda kwa kishindo lakini jina lake halikurudi.
"Tunawatakia kila la heri waliokosa uvumilivu, wako ambao hata uteuzi haujafanyika wakahamia mtaa wa pili siku ya tatu wakageuza tena CCM, niwape salamu hao waliowaokoteza tumewaazima tu wagombea, watarudi Chama Cha Mapinduzi.
"Kuna wengine hata vikao hatujakaa niliona wanakaribishwa siku mbili jamaa akarudisha kadi akarudi CCM, hivyo niwaombe kuweni watulivu, tuna uchaguzi mwakani," alisema Makalla.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED