UTAFITI umebaini Watu Wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi na Ukimwi (PLWHA) ni miongoni mwa makundi yanayokumbwa zaidi na magonjwa ya akili, ukiwamo wasiwasi kulinganishwa na makundi mengine.
Utafiti uliofanywa na Hospitali ya Rufani ya Kanda - Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na kuhusisha watu 593 (wanaume 164), umebaini kuna tatizo hilo.
Bingwa wa Magonjwa na Afya ya Akili KCMC, Dk. Frank Kiwango, akizungumza na Nipashe jana mara baada ya kuwasilisha andiko la utafiti kupitia Jumuiya ya Wadau wa Afya ya Akili Tanzania (TMH-CoP) ECHO, wasilisho likiandaliwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Kuna athari kwa wanaougua ugonjwa huo kwa sababu wanaweza kukata tamaa na kushindwa kutumia dawa zao za ARV, mtu akawa na wasiwasi zaidi na kitaalamu ataendelea vibaya. Kwa ujumla, maisha yatakuwa changamoto, hasa kwenye kuishi,” alisema. Dk. Kiwango alisema waliofanyiwa utafiti Septemba hadi Oktoba mwaka jana na matokeo kutolewa hivi karibuni katika kundi la PLWHA 593, watu 74 (asilimia 12) wana dalili ya ugonjwa wa wasiwasi, akisema ni idadi kubwa ambayo inahitaji kufikiwa kwa elimu.
“Ni kwa sababu watu wenye VVU wako hatarini kupata magonjwa hayo kama wasiwasi, sonona kwa hiyo tukaona kwa kuwa wamo hatarini na utafiti kadhaa wa nje umeonesha kwamba wako hatarini kuliko ambao hawana magonjwa sugu. “Tukaona tufanye utafiti kwenye eneo hilo. Tumefanya utafiti mjini Moshi, mkoa wa Kilimanjaro katika vituo vya CTC vinne, ambavyo vinatoa huduma za VVU.
KCMC; Hospitali ya Mkoa Mawenzi na vituo vya afya,” alisema. Bingwa huyo ambaye ndiye mtafiti mkuu kwenye utafiti huo, alisema baada ya kupata matokeo hayo, tayari mchakato wa kutoa elimu kupitia programu za afya elimishi umeanza, kama vile katika vyombo vya habari na makongamano.
“Wito kwa jamii ili kundi hili lisiingie katika tatizo, liweze kuangaliwa kwa jicho la ziada na kuwapo mpango endelevu wa kuchunguza magonjwa ya akili, ili kuwahi kupata huduma stahiki mapema,” alishauri. Alirejea ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2021 inayoonesha kuwa takribani watu wazima milioni 36 wanaishi na VVU/UKIMWI kwa mwaka huo. Kati yao, theluthi mbili wako barani Afrika. Pia PLWHA wapatao milioni 1.6 wanatoka Tanzania (WHO 2022).
Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Nuruel Kitomary, alisema kuwa na ugonjwa huo kunaweza kusababisha mtikisiko wa hisia, jambo linaloweza kuwasababishia watu wa kundi hilo kuathiri mtiririko wa matibabu. “Wasiwasi unaweza kushusha kinga ya amwili, tukumbuke pia wasiwasi kila binadamu anao ila ukizidi inapaswa kuingia katika matibabu. Kukaa kimya katika hili na ukosefu wa elimu kuna athari,” bingwa huyo alihadharisha.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED