PAMOJA na kufungwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC, Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ameeleza kufurahishwa kuongezeka kwa ushindani kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Gamondi, alisema kwa sasa kuna timu nne ambazo zina wachezaji bora, wenye uzoefu ambazo zinaweza kushinda mchezo wowote na kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.
Amezitaja timu hizo kuwa ni Simba, Yanga, Azam FC na Singida Black Stars, ambazo zimefanya usajili bora na kufanya vikosi vyao kuwa tishio.
"Msimu huu timu zimejipanga, zimekuwa bora, lakini kuna timu nne ambazo zina uzani wa juu na yoyote inaweza kuifunga timu yoyote na kuchukua ubingwa. Tumeona Azam imeshinda, ina wachezaji wazuri, Simba hali kadhalika ni timu bora msimu huu, halafu msimu huu imekuja timu nyingine ngumu nayo ni Singida Black Stars.
Timu hizi nne zimefanya kuongezeka kwa ugumu wa ligi na ubora, hivyo inabidi yeyote anayeutaka ubingwa kufanya kazi ya ziada," alisema Gamondi.
Hata hivyo, Gamondi alilalamikia mchezo wao dhidi ya Azam FC ambao kwa Yanga ulikuwa wa nyumbani kwenda kucheza kwenye uwanja wa wapinzani wao.
Alisema hakuona sababu mchezo huo kutochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kwa sababu wao ndiyo walikuwa wenyeji.
"Mimi sijafurahi kwa hiyo, niwe muwazi, kucheza mechi yetu ya nyumbani kwenye uwanja wa wapinzani wetu.
Wanasema Uwanja wa Benjamin Mkapa haiwezekani kucheza mechi mbili mfululizo kwa siku mbili, lakini nakumbuka msimu uliopita zilichezwa mechi mbili hapo hapo, tulicheza sisi mechi moja ya kimataifa leo na kesho yake Simba wakacheza pia, sina maana Uwanja wa Azam Complex ni mbaya hapana, ila kucheza mchezo wa nyumbani kwenye uwanja wa mpinzani wako ni kumpa faida," alisema Gamondi.
Alisema kwa sasa yamepita na anachoangalia ni kukiandaa kikosi chake kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Tabora United utakaopigwa kesho kutwa, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ukiwa ni wa kumi kwa timu hiyo.
Pamoja na kufungwa, Yanga bado inaongoza ligi ikiwa na pointi 24, ikifuatiwa na Singida Black Stars yenye pointi 23, Simba nafasi ya tatu na pointi zake 22, Azam FC ikisimama nafasi ya nne baada ya kukusanya pointi 21, huku Fountain Gate ikwa kwenye nafasi ya tano na pointi zake 17.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED