Ziwa Tanganyika kufungwa miezi mitatu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:37 PM Apr 02 2024
Ziwa Tanganyika.
PICHA: SHODOW OF AFRICA
Ziwa Tanganyika.

SHUGHULI za Uvuvi katika Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma zinatarajiwa kufungwa kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Mei 15 hadi Agosti 15, mwaka huu lengo likiwa ni kupumzisha ziwa hilo kupata ongezeko la samaki.

Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kukuza sekta ya Uvuvi nchini kwa kusaidia ongezeko la samaki ziwani humo.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salimu Kali wakati akizungumza na wadau, viongozi na wavuvi wanaotumia ziwa hilo na kutaja hatua hiyo kuwa pia sehemu ya kuongeza soko siku za usoni kutokana na uwapo wa samaki wa kutosha na wakubwa.

Kali amesisitiza umuhimu wa shuguli hiyo katika Ziwa Tanganyika na kusema kuwa kitovu cha mazao ya samaki hutokana na mazalia kuwa mengi na kukidhi mahitaji ya watumiaji.

“Sio tu kulipumzisha Ziwa Tanganyika, utafiti pia ulifanyika kwa nchi zote nne zinazotumia ziwa hili ikiwamo Tanzania, Kongo, Zambia na Burundi hivyo zilishirikiana na wakafikia makubaliano ya kulipumzisha kwa muda wa miezi mitatu kwa kila mwaka," amesema Kali.

Amesema walishirikisha viongozi wote wanaozunguka Ziwa Tanganyika kuanzia ngazi ya mtaa, wataalamu wa kuvua samaki pamoja na wazawa wa Kigoma na walitafuta muda ambao samaki wanapungua au kuisha kabisa ndio wakachagua miezi hiyo.

Katika hatua nyingine Kali amesema, wizara imekuja na suluhisho la kutengeneza vizimba kwa ajili ya ufugaji wa samaki pamoja na mbinu za kuwalisha samaki hao hivyo itasaidia pato la kila mmoja hususani kwa wategemezi wa shuguli ya uvuvi kwa ajili ya kujipatia kipato na pia itachangia pato la taifa.

“Tayari vizimba vimeshatengenezwa na mwezi Aprili vinatarajiwa kugawiwa kwa wavuvi kama utaratibu uliotumika kugawa vizimba Mkoa wa Mwanza kwa sababu hata hivi vizimba vimetengenezwa huko vikasafirishwa kuletwa Kigoma," amesisitiza.

Hata hivyo, Kali amewataka wananchi kuwa wasimamizi na walinzi wa vizimba hivyo kwa kuwa wao ndio wanufaika wa mradi huo na amewataka viongozi wa wavuvi kushirikiana na viongozi wa seikali kufanya kazi hiyo kuwa rahisi na kuleta tija kwa jamii inayolizunguka Ziwa Tanganyika.

Baadhi ya wavuvi wilayani humo wametaja hatua hiyo kuwa muhimu kutokana na ziwa hilo kupungukiwa mazao ya samaki wakati mwingine wakipatikana samaki wachanga na baada ya kipindi hicho wanatarajia kupata wakubwa na wenye thamani kubwa.