Watumishi walioathirika uhakiki taarifa, vyeti wapandishwa vyeo

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 09:47 AM May 21 2024
Naibu Waziri Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete.

WATUMISHI 375,904 wamepandishwa vyeo wakiwamo 85,471 walioathirika na uhakiki wa taarifa za kiutumishi na vyeti vya elimu kwa watumishi wa umma kuanzia mwaka 2021/22 hadi sasa, serikali imesema.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete, aliyasema hayo jana bungeni alipojibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu.

Mbunge huyo alihoji lini serikali itarekebisha madaraja ya watumishi wa umma, hasa walimu waliopandishwa na kunyang’anywa vyeo kuanzia mwaka 2016 hadi 2018 ili kupisha uhakiki wa wakati huo.

Akijibu swali hilo, Ridhiwani alisema kuwa mwaka 2016 serikali ilisitisha mambo mbalimbali ya kiutumishi ikiwamo upandishaji vyeo ili kupisha uhakiki wa taarifa za kiutumishi na vyeti vya elimu kwa watumishi wa umma.

"Katika kutatua changamoto zilizojitokeza kutokana na kusitishwa huko, mwaka 2021/22 serikali ilianza kutekeleza zoezi la kuwarejesha watumishi wa umma katika kada mbalimbali kwenye nafasi na vyeo vyao stahiki kwa njia mbalimbali ikiwamo msawazo wa vyeo na mserereko wa madaraja," alisema.

Ridhiwani alisema kuwa kwa mwaka 2023/24, serikali inatarajia kuwapandisha vyeo watumishi 81,503 wakiwamo walioathirika na zoezi la uhakiki wa taarifa na vyeti vya watumishi wa umma.