Vikwazo 370 uwekezaji na biashara vyafutwa

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 02:56 PM Apr 23 2024
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.
PICHA: MAKTABA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.

SERIKALI imetangaza kufutwa kwa tozo, ada na faini 374 zilizobainika kukwamisha shughuli za uanzishwaji wa biashara na uwekezaji ili kusaidia ongezeko la fursa za uwekezaji nchini.

Tozo hizo zinahusisha taasisi mbalimbali zikiwamo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Wakala wa Usalama Mahala pa Kazi (OSHA), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Hayo yamebainishwa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo kwa mwaka 2024/25.

Amesema pamoja na uondoshwaji wa tozo hizo, pia serikali imeunganisha mamlaka za urekebishaji ambazo majukumu yake yalionekana kuingiliana. Alitaja mfano wa majukumu hayo kuwa ni pamoja na majukumu yaliyokuwa chini ya TFDA yalihamishiwa TBS.

Pia amesema majukumu ya kutoa vibali vya kusafirisha kemikali yamehamishiwa kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, hivyo kuondoa mwingiliano uliokuwapo kati ya taasisi hiyo na TMDA pamoja na TANROADS. 

Aidha, amesema serikali imefanyia marekebisho ya Sheria ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Sura ya 415 ili kuondoa haki pekee (exclusive mandate) ya uondoshaji na usafirishaji (clearing and forwading) wa shehena kwa njia ya maji.

Amesema TASAC sasa inahusika na bidhaa nne pekee ambazo ni makinikia, wanyama hai, kemikali zinazotumika migodoni na nyara za serikali.

Prof. Mkumbo ameeleza kuongezeka kwa kampuni zinazosajiliwa kutoka kampuni 7,817 mwaka 2018/19 hadi kampuni 10,656 kwa mwaka mwaka 2021/22 pamoja na kuanzishwa kwa idara inayoshughulikia biashara, viwanda na uwekezaji katika mamlaka za serikali za mitaa.

VIPAUMBELE 2024/25

Kuhusu vipaumbele vya Wizara hiyo kwa mwaka 2024/25, Prof. Mkumbo amesema pamoja na mambo mengine, imepanga kukamilisha maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Pia amesema wanatarajia kukamilisha uandaaji wa sera mpya ya uwekezaji na mkakati wake wa utekelezaji pamoja na uunganishaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Maeneo ya Uzalishaji wa Mauzo ya Nje (EPZA)  na  kuanzisha  Taasisi  mpya  ya kusimamia masuala ya Uwekezaji wa sekta Binafsi.

Kadhalika, amesema wizara inatarajia kuendelea kusimamia utekelezaji wa mageuzi katika uendeshaji wa mashirika ya umma, ikiwamo kuendelea kubaini mashirika ambayo majukumu yake yamepitwa na wakati au yanaingiliana na majukumu ya taasisi zingine na kuchukua hatua stahiki, pamoja na kuweka vigezo bayana vya upimaji wa utendaji wa mashirika ya umma.

“Tutafanya mapitio ya sheria zinazohusu masuala ya madini, ardhi, kilimo, utalii na biashara kwa ajili ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Pia tunatarajia kuzindua na kutangaza mradi wa Bagamoyo SEZ kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa nia ya kuendeleza mradi kwa njia mbalimbali, ikiwemo ubia na sekta binafsi kwa kufuata mpango uliorejewa pamoja na kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi katika maeneo saba ya viwanda vilivyokabidhiwa kwa Mamlaka ya EPZ,” amesema Prof. Mkumbo.

Aidha, Prof. Mkumbo ameomba bunge kujadili na kuidhinishia wizara hiyo kutumia Sh. bilioni 121.329 kwa mwaka 2024/25 ambazo Sh. bilioni 100.246 ni kwa ajili ya  matumizi  ya  kawaida  na Sh.bilioni 21.08 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.