Samia aridhishwa na kazi za mabalozi nje ya nchi

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 06:19 PM Apr 23 2024
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
PICHA: MAKTABA
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

RAIS Dk Samia Suluhu Hassan amewapongeza Mabalozi wanaowakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani kwa kazi nzuri ya uwakilishi ambayo inaonekana kwa kuongezeka kwa masoko ya bidhaa za Tanzania, biashara, uwekezaji, utalii na tekbolojia nchini.

Rais Samia ametoa pongezi hizo alipokuwa anawahutubia Mabalozi hao kwa njia ya mtandao ambao wamekusanyika mjini Kibaha kwa warsha ya siku 4 ya kutathimini utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje iliyoanza Aprili 21 na itakamilika Aprili 24, 2024.

Amesema nchi inawategemea Mabalozi katika utekelezaji wa majukumu yao ili iweze kusonga mbele kiuchumi na kwa kuliona hilo, amesema amechukua hatua mbalimbali ili kuibadilisha Wizara ya Mambo ya Nje iwe ya kisasa zaidi na kuwa na uwezo wa kuitangaza nchi.

Lengo la Mabadiliko hayo ni kuifanya nchi iendelee kuheshimika na kuwa na ushawishi zaidi duniani kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma ya wakati wa harakati za ukombozi na baada ya ukombozi.

Amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuteua Naibu Waziri na Katibu Mkuu wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, kuanzisha Idara ya Diplomasia ya Uchumi, kusaini mikataba ya Kuzuia Utozaji wa Kodi mara Mbili na Kulinda Vitega Uchumi na nchi mbalimbali duniani, kuridhia mkakati wa uendelezaji wa majengo ya ofisi za Mabalozi na makazi na mchakato wa uboreshaji wa Sera ya Mambo ya Nje na Hadhi Maalum kwa raia wenye asili ya Tanzania wanaoishi Nje ya nchi ambao umefikia hatua nzuri.

Amewasihi Mabalozi kuwa jicho la Tanzania kwenye maeneo yao ya uwakilishi ili nchi isipitwe na Mabadiliko makubwa yanayotokea duniani. 

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kulinda Utamaduni wetu kwani kuna juhudi za makusudi zinazoendelea duniani za kulazimishwa tamaduni zilizo kinyume na maadili yetu.