Matumizi ya kijeshi yaongezeka duniani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:45 AM Apr 23 2024
Matumizi ya kijeshi yaongezeka.
PICHA: MTANDAO
Matumizi ya kijeshi yaongezeka.

TAASISI ya Kimataifa ya Utafiti wa Masuala ya Amani na Usalama (SIPRI), imesema matumizi ya kijeshi kote duniani yameongezeka kwa asilimia saba, ikiwa ni sawa na ongezeko la matumizi ya fedha ya dola trilioni 2.43 kwa mwaka 2023.

Taasisi hiyo ya SIPRI iliyoko mjini Stockholm, Sweden, imesema ongezeko hilo la asilimia saba ni kubwa tangu mwaka 2009 huku ikiongeza kwamba nchi kumi zilizokuwa na matumizi makubwa ya kijeshi kwa mwaka 2023 zimeongozwa na Marekani, China na Russia.

Nan Tian, Mtafiti Mkuu katika mpango wa uangalizi wa matumizi ya kijeshi na utengenezaji wa silaha wa SIPRI, amesema ongezeko linaloonekana limetokana na kudorora kwa amani na usalama wa dunia.

Amesema mataifa yanaweka mbele nguvu za kijeshi na matokeo yake ni kuhatarisha usalama wa dunia, akitolea mfano mataifa ya Russia kwamba imeongeza matumizi yake kwa asilimia 24 ambayo ni sawa na dola bilioni 109. Ukraine imeongeza kwa asilimia 51, sawa na dola bilioni 65 na kupokea angalau dola bilioni 35 za msaada wa kijeshi kutoka kwa Mataifa ya Magharibi.

“Nchi wanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO zimetumia takriban asilimia 55 ya matumizi ya kijeshi duniani,” imesema SIPRI.

Mtafiti mwengine wa SIPRI, Lorenzo Scarazzato, amesema miaka miwili ya vita vya Russia nchini Ukraine imebadilisha kabisa muonekano wa usalama na kutoa kitisho zaidi cha usalama badala ya amani na uthabiti duniani.

Katika Mataifa ya Afrika, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) iliongeza matumizi yake kwa asilimia 105, ikiwa moja ya nchi iliyo na matumizi makubwa mno ya kijeshi, mwaka 2023 na watafiti wanasema ongezeko hili bila shaka limetokana na mgogoro unaoendelea kati ya serikali, na makundi yaliojihami ya waasi.

Migogoro ya kikanda na uboreshaji wa kijeshi pia ni miongoni mwa mambo yaliyoongeza matumizi ya kijeshi, kwa mfano mgogoro kati ya China na Taiwan umetajwa katika ripoti hiyo kama moja ya vita vilivyoongeza matumizi ya kijeshi ya mataifa maeneo hayo mawili. Ikielezwa kuwa China, iliongeza matumizi yake kwa asilimia sita, huku Japan na Taiwan zikiongeza kwa asilimia 11.

Watafiti wa taasisi hiyo walisema wanakadiria katika utafiti watakaoufanya wa mwaka 2024 matumizi ya kijeshi huenda yakaongezeka zaidi kufuatia shambulizi la Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas katika Ukanda wa Gaza.

DW