Morocco afurahia kiwango nyota wapya Taifa Stars

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 09:03 AM May 21 2024
Kocha Mkuu wa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), Hemed Morocco.
Picha: TFF
Kocha Mkuu wa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), Hemed Morocco.

KOCHA Mkuu wa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), Hemed Morocco, amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wa timu hiyo katika mechi mbili za kimataifa za kirafiki zilizofanyika nchini Saudi Arabia.

Morocco amesema hayo baada ya Stars kumaliza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Sudan katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa King Fahad ulioko Taif, nchini humo.

Kocha huyo alisema katika mechi ya juzi wachezaji wake walibadilika na kuonyesha kiwango bora huku kila mmoja akijituma.

Alisema anaamini wachezaji hao wakipata mechi zaidi za kirafiki wataimarika na kuwa msaada zaidi katika kikosi cha timu hiyo.

“Ilikuwa ni mechi nzuri na ngumu, wachezaji wangu walianza taratibu lakini walibadilika kadri muda ulivyokuwa unasogea, waliamka na hatimaye kupata bao la kusawazisha,” alisema kocha huyo.

Aliongeza wachezaji hao wakiaminiwa na kupata uzoefu wa mechi za kimataifa, watakuwa ni nyota wa kutegemewa katika siku za baadaye kwa sababu hali ya kucheza kwa woga itawaondoka.

“Tukiwapa mechi nyingi na mechi hizo zikiwa za nje itakuwa jambo zuri katika mipango ya kuwaendeleza, pia tuwaamini, hii itawasaidia kuwajenga, wamekuwa tofauti katika mechi ya pili, wameanza kucheza kwa kuelewana,” aliongeza kusema Morocco.

Kikosi hicho kinajiandaa kurejea nyumbani baada ya kumaliza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Sudan.

Morocco alilazimika kuita wachezaji wengi wapya na chipukizi kutokana na nyota wakongwe kubanwa na ratiba ya michezo ya kumaliza msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya Kombe la FA ambayo hatua ya nusu fainali imemalizika juzi.