Wananchi wametakiwa kujitokeza kupata huduma ya matibabu bure

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 02:10 PM Jul 26 2024
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akikagua huduma za matibabu kwenye mabanda.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akikagua huduma za matibabu kwenye mabanda.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,amezindua rasmi kampeni ya utoaji matibabu bure kwa wananchi, huku akiwasihi kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma za matibabu kuimarisha afya zao.

Kampeni hiyo ya utoaji matibabu bure (Afya Code Clinic) imeratibiwa na Kampuni ya Jambo Group Limited kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ikishikwa mkono na Benki ya CRDB.

Macha, akizungumza jana wakati wa uzinduzi huo aliipongeza Kampuni ya Jambo kwa kushirikiana na serikali kuandaa huduma hiyo, ambayo itaimarisha afya za wananchi kwa kuwakutanisha pia na madaktari bingwa wakiwemo kutoka hospitali ya Agha-khan.

“Wananchi wa Shinyanga jitokezeni kwa wingi kwenye kampeni hii kupima afya zenu pamoja na kupata matibabu bure,” alisema Macha.

Aidha,alimpongeza pia Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za afya nchini na Mkoa wa Shinyanga ambapo kwa kipindi chake hadi sasa ametoa kiasi cha Sh.bilioni 30 na zimejengwa hospitali mpya zahanati na vituo vya afya lengo ni kuimarisha afya za wananchi.

1

Aliwata pia wananchi wa Shinyanga kukata kadi za bima za afya ambazo zitawasaidia pia kupata matibabu kwa urahisi pamoja na kujitoa kuchangia damu.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. Dk.Yudas Ndungile, alisema kampeni hiyo ya Afya Code Clinic inatolewa pia elimu za afya pamoja na uchunguzi wa magonjwa mbalimbali na hivyo kuwasisitiza wananchi wachangamkie fursa hiyo.

Naye Meneja Mkuu wa Jambo Media, Nickson Geogre, alisema  walizalisha wazo hilo kupitia vipindi vyao vya kijamii katika eneo la afya,ili jamii ipate kunufaika kwa kupata matibabu bure na wasikilizaji wao wawe na afya njema.
2

Nao baadhi ya wananchi ambao wamejitokeza kupata matibabu bure, wameishukuru kampuni ya jambo pamoja na Serikali, kuwapatia huduma hiyo na kuokoa afya zao.

Kampeni hiyo ya matibabu bure Afya Code Clinic imeanza julai 24 na itahitimishwa julai 27 mwaka huu ambayo ni siku ya Jumamosi.
3