Maandalizi NBC Dodoma Marathon yakamilika,wananchi watakiwa kuchangamkia fursa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:34 PM Jul 26 2024
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule  (wa pili kulia) akipokea sweta maalum la mbio za NBC Dodoma Marathon kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa Benki ya NBC, Godwin Semunyu (wa pili kushoto).
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule (wa pili kulia) akipokea sweta maalum la mbio za NBC Dodoma Marathon kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa Benki ya NBC, Godwin Semunyu (wa pili kushoto).

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amethibitisha kukamilika kwa maadalizi ya msimu wa tano mbio za NBC Dodoma Marathon huku akionyesha kuridhishwa na ubora wa mbio hizo sambamba na mchango wake katika kuchochea kasi ya Uchumi wa mkoa huo kupitia sekta za biashara, michezo na utalii.

Mbio zinatarajiwa kufanyika Julai 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma zikiwa na lengo la kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na  kutoa ufadhili wa elimu kwa wakunga  ili kuboresha afya ya mama na mtoto. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuongoza washiriki zaidi ya 8,000 waliothibitisha kushiriki mbio hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo RC Senyamule pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa maandalizi hayo mazuri alisema ujio wa mbio hizo mkoani humo kwa miaka mitano sasa umekuwa ukiambatana na fursa mbalimbali ikiwemo ongezeko la mzuguko wa fedha unaotokana na ongezeko la mahitaji ya chakula, vinywaji,mavazi na malazi kutona na idadi kubwa ya watu wanaotoka mikoa mbalimbali ili kushiriki mbio hizo jijini humo.

“Kukamilika kwa maadalizi ya mbio hizo tena katika viwango vya kimataifa kunatoa taswira sahihi ya hadhi ya mbio hizo na jiji la Dodoma kama makao makuu ya nchi. Nitoe wito kwa wananchi wa jiji la Dodoma hususani wafanyabiashara kuchangamkia fursa  mbalimbali zitokanazo na ongezeko hili la watu ambao nje ya washiriki hao 8,000 waliothibitisha  kushiriki pia wapo wengine zaidi walioambatana nao.’’  amesema.

Aidha, Senyamule aliowamba washiriki wa mbio hizo kutumia fursa hiyo pia kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyomo mkoani humo ukiwemo utalii wa majengo ya serikali kama vile Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ikulu, Mji wa serikali sambamba na utalii wa utamaduni ikiwemo ngoma za asili za wenyeji wa mkoa huo ambao ni kabila la Wagogo huku pia wakipata wasaa wa kujionea kilimo cha zao la zabibu ambalo kwa Afrika Mashariki linalimwa mkoa huo pekee.

“Zaidi nitoe wito kwa wananchi wajitokeze kwa wingi kandokando ya Barabara ili kushangilia na kuwapa nguvu washiriki wa mbio hizo watakaotumia baadhi ya barabara hapa mjini. Kwa wale ambao hawatakuwa na ulazima wa kutumia magari yao ni vema wasiingie nayo barabarani ili kupunguza msongamano wa vyombo hivyo barabarani ili kuepuka ajali na usumbufu kwa washiriki wa mbio hizi,’’ ameongeza.

Awali akizungumza kwenye mkutano huo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa Benki ya NBC, ambayo ndio inaratibu mbio hizo Godwin Semunyu alisema maandalizi yote yamekamilika na tayari washiriki mbalimbali wa mbio zinazohusisha umbali wa km 5, km 10,  km 21 na km 42 wanaendelea kuingia jijini humo ili kushiriki mbio hizo.

“Ili kuongeza mchango wa mbio hizi kiuchumi na burudani zaidi tumebuni matukio kadhaa likwemo tamasha la kuonja mvinyo yaani ‘Wine Testing Festival’ litakalofanyika Julai 27 hapa Dodoma na zaidi tumeandaa matukio mengine ya burudani za vichekesho na tafrija mbalimbali lengo likiwa ni kuongeza burudani wa washiriki wa mbio hizi hususani wageni huku pia tukilenga kuchochea mzunguko wa fedha ili kuwanufaisha zaidi wenyeji wa jiji hili,’’ alisema Semunyu huku akiwashukuru wadau mbalimbali wakiwemo wadhamini wa mbio hizo kufanikisha matukio hayo.

Akuizungumza kwa niaba ya wadau hao, Mkuu wa Kanda ya Kati wa Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania Joseph Sayi alisema kampuni hiyo ikiwa kama mdau mkuu wa mawasiliano kwenye mbio hizo imejipanga kutoa huduma ya mawasiliano ya internet bure kwa washiriki wote wa mbio hizo.