Watanzania tumeamua kuwa na nchi ya mawimbi!

By Joseph kulangwa , Nipashe
Published at 04:48 PM Jul 26 2024
news
Mchoraji: Msamba
Katuni.

UNAWEZA kusema Tanzania ni nchi ya mawimbi. Maana yake linaibuka wimbi hili, likishuka linaibuka lingine na kelele kibao, huku watu wakilaumiana na kukosa la kufanya.

Miaka ya nyuma liliibuka wimbi la mauaji ya vikongwe, wazee hususan wa kike walioonekana kuwa na macho mekundu, wakihusishwa na masuala ya ushirikina. Mikoa ya Kanda ya Ziwa hususan Shinyanga, ilihusika sana.

 Wimbi hilo lilipigiwa kelele na serikali ikiwataka wanajamii kushirikiana nayo kupitia vyombo vya usalama kuyakomesha, hatimaye aliyekuwa bosi wa vyombo hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ali Hassan Mwinyi, akajiuzulu. 

Mwinyi alijiuzulu uwaziri huo Julai 1976 nasi kutokana nayeye kushiriki mauaji hayo, la hasha, bali aliwajibika kutokana na kwamba alikuwa ndiye msimamizi mkuu wa usalama wa raiana mali zao. 

Hata hivyo, wimbi hilo halikushuka, liliendelea huku bibi na babu zetu wakiuawa kinyama tu, tena wauaji wengine wakiwa ni ndugu wa karibu, kwa sababu tu ya imani hizo potofu. 

Baada ya mapambano ya muda mrefu, wimbi likashuka, lakini likaibuka, likapisha lingine hili likilenga wenye ulemavu wa ngozi, yaani ualbino.  

Wauaji kwa imani hiyo hiyo ya kishirikina, wakikata viungo vyao na kuvitumia visivyo. Imani ikiwapeleka kwenye utajiri, kwamba unakata kiungo chamwenye ualbino, unakipeleka kwa mganga wa kienyeji, anakufanyia ayajuayo na wewe kama ni mchimba madini unatajirika, kama ni mkulima unatajirika na kama ni mwanasiasa unashinda uchaguzi. 

Uovu huo pia kama wa mauaji ya vikongwe, ukifanywa na watu wa karibu wa na waathirika. Nchi ikaingia kwenye kimuhemuhe, watu wakikamatwa na voiungo na kufunguliwa mashitaka na kufungwa. 

Lawama nyingi zikaelekezwa kwa waganga wa jadi waliorubuni watu kuwa wanawatengenezea dawa hizo, lakini kumbe wakiwakamua fedha na wao kujitajirisha huku wauaji wakiendelea kubaki masikini kama zamani.

 Mapambano ya serikali kupitia vyombo vyake, ikishirikiana na wananchi ikashusha wimbi hilo, mauaji hayo yakajipumzisha kidogo mpaka yailivyokuja kuibuka tena mwaka huu, maeneo ya mkoani Kagera. 

Katikati hapo likaibuka wimbi, lingine la wasiuojulikana kwamba ni watu wasio na sura, wakiteka wenzao na kuwapoteza ama kwa kuwaua au kuwafanya vinginevyo kusikojulikana. 

Kasikia majina ya wanasiasa, wanahabari na wafanyabiashara wakitekwa na wasiojulikana na baadhi yao wakirejea wamejeruhiwa au wakiokotwa wakiwa taabani, lakini wengine mpaka leo hawajulikani waliko.

Mabadiliko ya uongozi wa taifa hili yakatuaminisha kuwa, pengine wasiojulikana,  hawa nao walitoweka na awamu iliyopita, lakini kumbe walikuwa wakisubiri muda wao ufike wana kuibuka na wimbi hili lingine. 

Hivi sasa ni mshikemshike mitaani katika maeneo mbalimbali nchini, watoto wakitekwa na kupotezwa, wengine wakijeruhiwa na baadhi kuuawa! Sababu yake mpaka sasa haijulikani, inabaki tetesi tu. 

Kinachoshangaza na kusikitisha, vyombo vya usalama badala ya kuibuka na kuingia kazini kusaka wanaofanya haya, vinasigana na kuvinatupa lawama kwa wananchi wanaolalamika vikisema ni uongo na nia mbaya ya kuzusha, sintofahamu na taharuki mitaani. 

Lakini, vyombo vya habari navyo vinagoma na kuingia mitaani na kutonesha mbashara yanayofanyika mitaani, ambako taharuki imewakuita wenye uchungu, wenye watoto wao.  

Wazazi wakiona wenzao wananyolewa nao wanaamua kutia maji nywele zao, kwani kunyolewa kunawakaribia, wakiumwa na nyoka wanaogopa nyasi, hivyo kuzua malalamiko kila kona na kuogopa watu kusogelea watoto wao. 

Ni vizuri viongozi wa Jeshi la Polisi nchini. akajiridhisha na hali ilivyo badala ya kuibuka na kusema hakuna kitu kama hicho, bali ni uzushi mtupu unaosababisha taharuki kwa wananchi, wakiwataka kutulia na kuendelea na maisha yao. 

Hivi mtoto wa mtu akitekwa na kufanyiwa uovu ikiwa ni pamoja na kulemazwa kama si kuuawa, nani analipa fidia hiyo? Ni vema kujiuliza kulikoni kabla ya kuhitimisha kirahisirahisi. 

Yawezekana kuna biashara ya viungo inafanyika ndani au nje ya nchi na tetesi zikisema figo ina soko kubwa, tunadhani wanaosaka fedha wafanyaje kama wanaona kuna bidhaa inayopatikana kwa kuteka Watoto watu?

 Tumeamua nchi kuwa ya kamari, hivi sasa kila kona ya nchi kuna michezo ya kubahatisha, hakuna kituo cha redio kisicho na mchezo wa kubahatisha, lipa Sh 1,000 ujipatie maelfu kwa mamilioni ya fedha!

Nani ataacha kubeti na kucheza bahati nasibu au kamari, akaenda kumtafuta Hussein Bashe na mashamba yake ajiunge na kilimo cha BBT?  

Kama pesa inapatikana kupitia umekaa nyumbani ukisubiri simu uwe kwa mshindi wa ‘Mshua’, kwanini usijaribu na kuteka mtoto ujipatie figo? 

Watanzania tuamke, tuache kusaka utajiri rahisi na wa haraka tutaangamizana bure. Fuatilia anayocheza bahati nasibu hizo, utakuta ni walalahoi wasio na kitu! Kwanini? Usinijibu tafadhali.